Beki wa Pembeni wa Young Africans Shomari Kibwana amekubaki kiwango cha Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Bernard Morrison, baada ya kupambana naye kwenye mchezo wa Ligi Kuu Jumamosi (Desemba 11).

Simba SC ilikuwa mwenyeji wa Young Africans, Uwanja wa Benjamin Mkapa, katika mchezo wa mzunguuko wa nane ambao ulimalizika kwa sare ya 0-0.

Shomari ambaye anaitumikia Young Africans kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kusajiliwa kutoka Mtibwa Sugar, amesema Morrison ni mchezaji mchachari na wakati wote ana lengo la kufanya maajabu ili aisaidie timu yake kupata ushindi.

Amesema Kiungo huyo ambaye aliwahi kuitumikia Young Africans kama akikutana na beki mwepesi anaweza kumuumbua kutokana na udambwidambwi wake uwanjani.

“Morrison ana akili kubwa ya mpira, jambo linalowafaidisha Simba kuwa na uhakika wa mtu anayeweza akawatengenezea nafasi za kupata matokeo. Ukimzuia huku unamkuta kule, kiukweli jamaa ana mpira mwingi mguuni kwake,” amesema Shomari.

“Nazungumza hayo kwani nimeshuhudia makali yake kwa kukabana naye kwenye dabi ya Desemba 11, nilikuwa namuona hapa mara namuona yupo kule, pia anajua kuuficha mpira mguuni kwake.” ameongeza Shomari

Licha ya kuonesha machachari kwenye mchezo dhidi ya Young Africans, Morrison alishindwa kuisaidia Simba SC kuchomoza na ushindi kwenye mchezo huo kama alivyofanya walipokutana dhidi ya Red Arrows ya Zambia.

Katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika, Morrison alifunga mabao mawili kati ya matatu, huku akikosa mkwaju wa penati.

Bunge lapitisha matumizi ya BANGI
Simba SC kuifuata Kagera Sugar