Meneja wa Klabu Bingwa nchini England Manchester City Pep Guardiola amemlinganisha Mshambuliaji Sergio Aguero na wababe wa Argentina Diego Maradona na Lionel Messi baada Gwiji huyo kutangaza kustaafu soka jana Jumatano (Desemba 15).
Aguero mwenye umri wa miaka 33 ametangaza kuacha kucheza soka kutokana ugonjwa wa moyo unaomkabili kwa sasa.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester City, alifunga zaidi ya mabao 400 katika kipindi chake cha miaka 18 na pia alichezea Atletico Madrid na Independiente. Aliichezea Argentina michezo 101.
“Maradona aliishinda Italia, Messi alifanya hivyo Uhispania na Aguero amefanya hivyo huko Uingereza, idadi yake inajieleza,” Guardiola aliiambia ESPN Argentina.
Aguero aliisaidia Argentina kushinda Copa America 2021 – taji lao la kwanza kuu ndani ya miaka 28, na Messi alitoa pongezi kwa mshambuliaji huyo kwenye ukurasa wake wa Instagram.
“Ukweli sasa inauma sana kuona ni kwa jinsi gani unapaswa kuacha kufanya kile ambacho unakipenda zaidi kwa sababu ya kile Kilichotokea kwako,” Messi amesema.
“Tuliishi nyakati nzuri sana na zingine ambazo hazikuwa nyingi, zote zilitufanya kuwa na umoja zaidi na zaidi. Tutaendelea kuishi pamoja nje ya dimba.”