Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGOs) katika shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Waziri ameyasema hayo leo Desemba 17, 2021 wakati akifungua Kongamano la Kukomboa Ardhi iliyochakaa katika Nyanda kame za Tanzania sanjari na Maadhimisho ya miaka 10 ya Shirika la Lead Foundation.
Amesema kuwa kongamano hilo linatoa taswira ya namna gani NGOs zinashiriki kikamilifu katika kusukuma mbele agenda ya mazingira nchini hivyo kuwajengea uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda na kuhifadhi mazingira.
“Niliwahi kuitisha mkutano na mashirika yanayojihusha na suala zima mazingira na leo najisikia faraja kubwa kuona mashirika haya yanapiga hatua na lengo langu kubwa ni kuona kila mmoja anashiriki katika suala zima la uhifadhi wa mazingira,” Amesema Waziri Jafo.
Aidha Waziri Jafo amesema Serikali itaendelea kusimamia Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira inayowashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wadau kutoka mashirika hayo.
Amesema anafarijika kutokana na Mpango Mkakati wa miaka 10 uliozinduliwa na Lead Foundation ambao unaonesha namna gani linaunga mkono Serikali katika hatua za kutunza na kuhidhi mazingira hususan katika eneo la mabadiliko ya tabianchi linaloikabili dunia.
Kwa upande mwingine ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wananchi kutumia kipindi hiki cha masika kupanda miti kwa wingi na kuitunza ili kukabiliana na ukame ambao huleta athari mbalimbali za kijamii.