Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatoa ushirikiano kwa Serikali ya Jamhuri ya Zimbabwe kutambua maeneo yote ambayo yalitumiwa na wapigania uhuru wa Zimbabwe kwa lengo la kutunza historia ya nchi hizo mbili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Waziri Bashungwa amesema hayo leo Desemba 17, 2021 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Habari na Utangazaji wa Jamhuri ya Zimbabwe Monica Mtsvangwa jijini Dodoma.

Ziara ya Mutsvangwa nchini inalengo la kutambua, kukusanya na kuhifadhi taarifa na kumbukumbu za harakati za ukombozi wa Zimbabwe zilizopo hapa nchi katika mfumo wa kidigitali.

Kwa upande wake Waziri wa Habari na Utangazaji wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Monica Mtsvangwa ameishukuru Tanzania kwa kutenga na kuanzisha maeneo ya kambi za kuwaandaa wapigania uhuru wa nchi yao na wanaamini watapata taarifa ambazo zitawasidia kutengeneza makala maalumu ya historia ya ukombozi wa taifa lao yatakayotumika kutoa elimu kwa wananchi wa Zimbabwe.

Maeneo ambayo msafara wa Waziri Mhe. Mutsvangwa watayatembelea ni Nachingwea mkoani Lindi, Mgagao mkoani Iringa, Kongwa mkoani Dodoma, Chunya mkoani Mbeya na Bagamoyo mkoani Pwani.

Mchengerwa awaonya viongozi wanaokiuka haki ya likizo
Rais Samia azungumza na walimu nchini