Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa amesema likizo ni haki ya mtumishi kisheria, hivyo hakuna haja ya Kiongozi kuzuia haki hiyo isipokuwa kwasababu maalum ambayo mtumishi husika atashirikishwa.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF Mkoani Geita.
Amesema kuwa, Kiongozi anapotaka kuzuia likizo ya mtumishi, afuate taratibu ambazo ni pamoja na kuzungumza na Mtumishi husika anayetaka kuchukua likizo aidha, kwa kumlipa gharama za kuzuia likizo hiyo au kumsogezea muda wa kuchukua likizo hiyo.
Aidha amewataka Viongozi kuwa na utamaduni wa kusoma nyaraka mbalimbali za kiutumishi ili kujua sheria na taratibu zitakazowasaidia kuwaongoza pale wanapotaka kutoa matamko yanayozuia stahiki za mtumishi.
amesisitiza kuzungumza na mtumishi kwa kutumia lugha nzuri na akakuelewa kuliko kutumia cheo ulichonacho au lugha kali kwani unaweza ukazuia likizo yake na asifanye kazi inavyotakiwa.
“Sisi Viongozi tujitahidi sana kujenga matumaini kwenye mioyo ya watumishi tunaowaongoza, tuwasikilize na kutatua kero zao, tuwe karibu nao ili wasiwe waoga na hatimaye kupoteza ubunifu walio nao katika utendaji kazi wao,” Amesema Waziri Mchengerwa.