Kamanda wa polisi Mkoani humo ACP Blasius Chandata, amesema Jeshi hilo limekamata Lita 4,135 za mafuta aina ya Diesel ambazo zinadaiwa kuibiwa kutoka kwenye Mradi wa ujenzi wa reli ya Kisasa (SGR) eneo la Malampaka Wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu.
Akizungumza na waandishi wa habari ACP Chandata amesema kuwa mafuta hayo yanakadiliwa kuwa na thamani ya Sh. 10,668,300 ambapo yalikutwa yakiwa yamehifadhiwa kwenye Mapipa 10 yenye ujazo wa Lita 200 kwa kila Pipa.
Kupitia msako mkali uliofanyika katika eneo la mradi huo mnamo Desemba 17, 2021 majira ya saa tano usiku, mbali na kukamatwa kwa mafuta hayo, ilikamatwa pia mifuko ya Saruji 28 aina ya Simba yenye thamani ya Sh. 616,000 pamoja na pikipiki tatu ambazo zinadaiwa kutumika kubeba mizigo hiyo ya wizi.
Licha ya kukamatwa kwa vitu hivyo, mtuhimiwa aliyejulikana kwa jina la Bundala Sambayi anayedaiwa kuhusika katika wizi huo aliweza kutoroka ambapo jeshi hilo la polisi limemtaka kujisalimisha mwenyewe mara moja.
“ Mengine yalikuwa kwenye dumu moja lenye Ujazo wa lita 50, madumu 25 yenye ujazo wa Lita 20 kila dumu, madumu 25 yenye ujazo wa lita 25 kila dumu, madumu 32 yenye ujazo wa Lita 30 kila dumu, mpira mmoja wa kunyonyea Mafuta, Fanel Moja, Majaba 2 tupu, Mapipa Matatu tupu” amesema Kamanda Chatanda.
Amesema kuwa Bundala Sambayi ambaye ndiye mmiliki wa nyumba iliyokutwa mali hizo na mhusika alitokomea kusiko julikana ambapo jitihada za kumtafuta zinaendelea.