Vinara wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans huenda wakasajili Beki wa Kati ambaye atasaidiana na Dickson Job na Bakari Mwamnyeto ambao ndiyo tegemeo kwa sasa.
Young Africans inatajwa kuwa sehemu ya klabu za Ligi Kuu ambazo zipo sokoni kusaka baadhi ya wachezaji katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la Usajili ambacho kimefunguliwa tangu Desemba 16, mwaka huu na kutarajiwa kufungwa Januari 15, mwakani.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Young Africans, Thabiti Kandoro amesema mipango ya klabu yao kwa sasa ni kuhakikisha wanapata beki mmoja wa kati ambaye atawasaidia Mwamnyeto na Job.
Kandoro amesema viongozi wametazama kikosi na kupitia ripoti ya benchi la Ufundi, wamegundua ili kudumu kwenye ubora walionao sasa ni vema wakasajili beki mmoja wa kati.
“Tunahitaji kuwa na timu iliyotimia kwenye kila idara, ukitazama kwa umakini utagundua Yanga inahitaji kuwa na beki mwingine wa kati, kariba ya kina Mwamnyeto na Job.
“Lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo mzito wale wachezaji, hiyo itasaidia timu kuwa na ubora ule ule ambao sisi tunahitaji kuona kwenye kila mechi,” amesema.
Young Africans inaendelea kuongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 23, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 18.