Mashabiki na Wanachama wa Simba SC Mkoani Tabora wameipokea kwa shangwe timu yao, baada ya kuwasili mkoani humo leo Jumatano (Desemba 22) majira ya mchana.
Simba SC imewasili mjini Tabora tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa kumi wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaowakutanisha dhidi ya KMC FC, Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi Ijumaa (Desemba 24).
KMC FC imechagua Uwanja wa Alli HAssan Mwinyi kama Uwanja wao wa nyumbani kwa ajili ya mchezo huo, wakitumia kanuni za Ligi Kuu ambazo zinatoa nafasi kwa timu shiriki kucheza nje ya Uwanja wao kwa michezo isiyopungua miwili kwa msimu.
Hii ni mara ya pili kwa KMC FC kucheza nje ya Dar es salaam, baada ya kufanya hivyo kwenye mchezo dhidi ya Young Africans uliopigwa mjini Songea mkoani Ruvuma kwenye Uwanja wa Majimaji mwezi Oktoba.
Simba SC itacheza mchezo huo Ijumaa (Desemba 24), baada ya mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar kuahirishwa siku ya Jumamosi (Desemba 18) mjini Bukoba, kufuatia asilimia kubwa ya wachezaji wake kuugua ghafla mafua makali.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 18 baada ya kucheza michezo minane, huku KMC FC ikiwa nafasi ya tisa kwa kufikisha alama 10.