Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekipiga faini ya Sh2 milioni Kituo cha Televisheni cha Wasafi kwa kosa la kurusha maudhui yasiyo na staha yaliyo kashifu na kuleta tafsiri potofu kuhusu imani ya dini ya kikristo.
TCRA imetoa onyo kali na kukiamuru kituo hicho kuomba radhi watazamaji wake na umma kwa kipindi cha siku tatu kuanzia Desemba 23 hadi 25 na mara tatu kwa siku kila baada ya saa nne kwa kosa hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui, Habbi Gunze ametoa hukumu hiyo leo Desemba 22, 2021 ameeleza maudhui hayo yalirushwa na Wasafi kupitia mtandao wakwa YouTube, yenye kichwa cha habari “Hata Yesu alifuata wenye pesa msituite matapeli.”
“Baada ya kutafakari kamati imeridhia pasipo na shaka kwamba, Wasafi televisheni kupitia kipindi chake chake hicho imekiuka kanuni za mawasiliano ya kieletroniki na posta maudhui ya mtandaoni 2020 kama ilivyowasilishwa katika tathmini ya kamati,” amesema.
Aidha Gunze, amesema kipindi hicho kilitangazwa kupitia mtandao wa YouTube ya Wasafi Novemba Mosi mwaka huu na mtangazaji Jordan Mwasha (Mchaga OG) ambaye alikuwa akifanya mahojiano na mtu anayejiita Nabii Daniel Shillah.
Gunze amesema kipindi hicho kimerushwa pasipo kuzigatia sheria, kanuni na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari.