Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC limetamba kuondoka na alama tatu muhimu mbele ya KMC FC, kwenye mchezo wa Ligi Kuu utakaopigwa kesho Ijumaa, Uwanja wa Alli Hassn Mwinyi mkoani Tabora.
Simba itakua mgeni katika mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa soka mkoani Tabora na mikoa ya jirani, ambao walionekana kuhamasika baada ya kikosi cha Mabingwa hao kuwasili jana Alhamis (Desemba 23) mchana kwa usafiri wa Ndege.
Kocha Msaidizi wa Simba, Thierry Hitimana, amesema wamekiandaa kikosi chao vizuri kuelekea mchezo huo, na wanaamini mambo yatakua mazuri baada ya dakika 90.
Hitimana amesema pamoja na kutarajia matokeo mazuri bado hali za wachezaji wao hazijaimarika vyema, lakini leo Alhamis (Desemba 23) watakamilisha maandalizi ya kuwakabili KMC FC kesho Ijumaa (Desemba 24).
“Hivi karibuni tumekutana na changamoto za maradhi lakini tunaendelea vizuri na tumesafiri salama hadi Tabora, na tuko tayari kwa ajili ya kupambana kutafuta matokeo chanya katika mchezo wetu huu muhimu,”
“Tumejiandaa vizuri licha ya kuwakosa baadhi ya nyota wetu kama John Bocco, Bernard Morrison na Erasto Nyoni ambao bado wanaumwa, habari nzuri ni kurejea kikosini kwa Rally Bwalya ambaye hakuwepo katika kikosi kilichoenda Kagera,” amesema Hitimana.
Kocha huyo amesema kutokana na changamoto waliyokuwa nayo, wanatarajia kufanya mabadiliko katika kikosi chao kwa kutoa nafasi kwa wachezaji ambao hawakuonekana sana katika mechi zilizotangulia za timu hiyo ambayo bado inashiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ameongeza wanafahamu ligi hiyo imekuwa na ushindani na kwa sababu hiyo, kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza atatakiwa kujituma na kupambana ili kufikia malengo.
“Tunaimani hadi kufikia Ijumaa wachezaji wetu watakuwa wameimarika zaidi, wanafahamu wanatakiwa kupambana ili kuvuna pointi, mechi haitakuwa nyepesi kwa sababu timu zote ni ngumu,” Hitimana amesema.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 18 baada ya kucheza michezo minane, huku KMC FC ikiwa nafasi ya tisa kwa kufikisha alama 10.