Kocha Mkuu wa klabu ya Young Africans Nasreddine Nabi, amesema anaamini Uongozi wa klabu hiyo utahakikisha unawanasa nyota wote aliowapendekeza katika ripoti yake katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo la usajili, ambalo limeshafunguliwa ili kufikia malengo waliyojiwekea katika msimu huu wa 2021/22.

Kocha kutoka nchini Tunisia amesema endsapo mpango huo utafanikiwa, anaamini kikosi chake kitaimarika zaidi na kuendelea kupata matokeo chanya katika kila mchezo watakaocheza msimu huu 2021/22.

Amesema amependekeza usajili wa wachezaji ambao ana uhakika watakua chachu ya kuongeza juhudu kwenye kikosi chake, ambacho msimu huu kimedhamiria kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara.

“Nimependekeza usajili wa wachezaji wenye sifa za kuitumikia klabu hii, ninaamini wachezaji wote wakisajiliwa wataweza kuleta chachu ya kufanikisha lengo tunalolikusudia msimu huu.”

“Dhamira yetu ni kuwa na kikosi imara ambacho kitapambana bila kukata tamaa, najua nikiwa na wachezaji wenye ari ya kushindana kuna kitu tutapata na kila mmoja wetu atafurahi.” amesema Kocha Nabi

Young Africans imeweka wazi itasajili wachezaji wapya ‘kimkakati’ na si kukurupuka kwa sababu tayari ina kikosi imara ambacho kimeanza msimu vizuri.

Hadi sasa klabu hiyo imeshacheza michezo tisa ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ikiongoza msimamo wa ligi hiyo kwa kufikisha alama 23, baada ya kushinda mchezo wake dhidi ya Tanzania Prisons mabao 2-1, siku ya Jumapili (Desemba 19).

Nketiah afunguka ushindi wa Arsenal
Azam FC kujiuliza kwa Ruvu Shooting