Baada ya kuifungia Arsenal Mabao Matatu ‘Hat-Trick’ kati ya Mabao Matano kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Ligi (Carabao Cup), Mshambuliaji Kinda Eddie Nketiah, ametoa shukurani kwa wachezaji wenzake.

Nketiah aliyekua kwenye kiwango cha hali ya juu katika mchezo huo dhidi ya Sunderland uliopigwa Juzi Jumanne (Desemba 21), amesema alichokifanya sio ujanja wake pekee, bali ni umoja na mshikamano uliopo kwenye kikosi cha Arsenal kwa sasa.

Mshambuliaji huyo amesema: “Ni hisia nzuri sana kwangu. Napenda tu kuwashukuru wachezaji wenzangu.

“Nilipata asisti nzuri sana, nilichotakiwa ni kuwa tu katika sehemu sahihi. “Ni jambo zuri kupata hat-trick yangu ya kwanza kwa timu ya wakubwa ya Arsenal.

“Haya ni mashindano ambayo mara zote nimekuwa nikipata nafasi ya kuanza na kupata nafasi kubwa zaidi ya kucheza.”

Nketiah alifunga bao la kwanza akiunganisha mpira uliopigwa na Rob Holding kabla ya kufunga mengine mawili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 sasa amefikisha mabao 10 katika michezo tisa aliocheza, saba zikiwa kwenye dimba la nyumbani ‘Emirates Stadium’.

WHO yaonya chanjo ya nyongeza
Nabi atarajia makubwa Young Africans