Mamlaka ya udhibiti usafiri ardhini LATRA imesema haijapandisha nauli za mabasi katika msimu huu wa sikukuu na kuwaasa wasafiri wote kuwa makini na walanguzi wa tiketi za mabasi.

Akiongea katika mahojiano maalumu na Dar24 media Mkurugenzi wa udhibiti usafiri wa barabara, Johansen Kahatano amewataka wasafiri wote kuwa makini na upandishwaji holela wa nauli ambao haujatolewa na mamlaka.

“kuna walanguzi wa tiketi ambao wananunua tiketi nyingi za mabasi tofauti, na kuwauzia abiria kwa bei ya juu ilhali ndani ya tiketi hiyo wanaandika bei ambayo ni elekezi” amesema Kahatano.

Ameongeza kuwa katika kupunguza tatizo hili la msongamano wa abiria hasa kipindi hiki cha msimu wa sikukuu, mamlaka imeanzisha mfumo wa tiketi mtandao ambao ulianzishwa rasmi januari mwaka 2021 lakini ulisimama kutokana na changamoto kadhaa.

“mfumo huu utaanza rasmi tena mapema mwakani kwa sababu siku za karibuni kamati iliyoundwa na Wizara imepeleka taarifa rasmi kwa naibu waziri wa Uchukuzi na baada ya hapo yale mwaswala yaliyotajwa yatafanyiwa kazi ili mfumo utakapoanza uwe na muendelezo” ameongeza Kahatano

Kuhusiana na swala la upungufu wa mabasi msimu huu wa sikukuu mamlaka inatoa vibali kwa mabasi ambayo yanaweza kusafiri mwendo mrefu na mikoa ambayo ina uhitaji mkubwa kwa sharti la kuwekewa kifaa cha kufuatilia mwendo wa basi “tracking Device”

Aidha Mkurugenzi huyo amewataka wasafiri wote amabo watapata shida ya ulanguzi wa tiketi wapige simu namba 0800110019 kwa msaada na pia kwa haraka zaidi maeneo yote ya stendi kuna maafisa wa mamlaka ambao wamevaa makoti yenye nembo ya mamlaka, hao wanaweza kutoa msaada wa haraka.

Mamlaka ya Usafiri Ardhini LATRA hutoa taarifa za nauli elekezi kwa wasafiri wote katika mabango makubwa ambayo huwekwa katika milango mikuu ya stendi kubwa na kwa sasa msafiri anaweza kuangalia nauli hizo katika mtandao wa www.latra.com ili kuwa na uhakika wa nauli ya eneo analokwenda.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Disemba 24, 2021
Rais Samia afanya uteuzi