Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wameanza kupanga karata zao kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaopigwa Jumamosi (Januari Mosi 2022), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Simba SC itakua mwenyeji kwenye mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki soka nchini, baada ya kuibanjua KMC FC mabao 4-1, mjini Tabora katika Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi.
Akizungumzia maandalizi ya kuelekea mchezo dhidi ya Azam FC, Kocha Msaidizi Hitimana Thiery amesema wamedhamiria kushinda mchezo huo, ambao amekiri utakua na changamoto kubwa ya ushindani.
Hitimana amesema anatarajia mchezo huo utakuwa wa ushindani mkubwa kwa sababu kila mmoja wao anahitaji matokeo chanya, lakini wao wanazihitaji zaidi alama tatu kuelekea kutimiza malengo yao ya kutetea ubingwa.
Amesema malengo yao ni kuhakikisha wanapata alama tatu katika kila mchezo wa ligi ili kujihakikishia kutetea ubingwa wao kwa mara nyingi kwa msimu huu.
“Ligi imekuwa ngumu na ushindani ni mkubwa, kila mmoja anahitaji kupata matokeo chanya, hivyo Pablo amewasisitizia wachezaji kutochelewa kurejea kambini kwa ajili ya kuendelea pale tulipoishia kuelekea mchezo wetu dhidi ya Azam FC,” amesema Hitimana ambaye kwa pamoja na Selemani Matola ni wasaidizi wa Kocha Franco Pablo Martin.
Simba SC inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 21, huku Azam FC, ambayo imeshashuka dimbani mara 10 msimu imejikusanyia alama 15 zinazoiweka nafasi ya saba.
Baada ya mchezo huo, Simba SC, Young Africans, Azam FC na Namungo FC zitaelekea Zanzibar tayari kwa michuano ya Mapinduzi Cup inayotarajiwa kuanza Jumapili (Desemba 02).
Simba SC ipo Kundi C pamoja na Selem View na Mlandege FC, wakati Kundi B, linaundwa na Young Africans, Taifa Jang’ombe na KMKM SC huku Kundi A likiwa na Azam FC, Namungo, Yosso Boys na Meli 4 City.