Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amejibu kauli ya tahadhari iliyotolewa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa ‘nchi inaweza kupigwa mnada’ endapo deni la taifa litazidi uwezo.
Akizungumza leo kupitia Clouds Fm, Profesa Luoga amesema kuwa Tanzania iko katika hali nzuri katika kiwango cha deni la taifa na kufafanua kuwa haiwezekani nchi ‘kupigwa mnada’ kutokana na kuzidiwa na deni.
“Nchi kupigwa mnada..! Si nchi nyingi zingekuwa zimechukuliwa na nchi nyingine. Lakini suala la mikopo ya nchi linachukuliwa kwa umakini mkubwa, na ndio sababu mikopo yote ya nchi inasajiliwa Benki Kuu ili tufahamu tuko katika hali gani na kushauri,” alisema Profesa Luoga.
Gavana huyo wa Benki Kuu alifafanua kuwa kipimo cha hali ya mikopo hupimwa kwa kuangalia kiwango cha GDP (Gross Domestic Product), na kwamba kiwango kizuri kwa kiwango cha kimataifa ni kile kisichozidi wastani wa asilimia 40, na kwamba Tanzania sasa iko katika asilimia 17 tu.
“Katika nchi 170, Tanzania iko kwenye namba 109 kwenye msimamo wa deni ukilinganisha na GDP. Katika Afrika Angola ndio inaongoza ikiwa na 101%,” alisema.
“Kwa Tanzania, kwa upande wa kiwango cha uhilivu wa deni ulipaswa usizidi asilimia 70 (threshold), lakini Novemba 2020/21 Tanzania tulikuwa kwenye asilimia 27.9, na mwaka huu tulipima tena uhilivu wa deni na tunaamini haitafika hata asilimia 28.5,” aliongeza.
Profesa Luoga aliendelea kufafanua kuwa katika viwango vya mikopo ya nchi, Tanzania bado iko kwenye rangi ya kijani lakini zipo nchi zilizoendelea zaidi ambazo ndizo ziko kwenye rangi nyekundu, ikimaanisha kuwa ndizo zinazokopa zaidi.
“Nchi zinazokopa sana ni zile ambazo zina uwezo mkubwa. Kwenye kiwango kwa mfano, Japan wana deni la zaidi ya asilimia 200 ya GDP,” alisema.
Aidha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania alisisitiza kuwa kwa utaratibu wa Tanzania, nchi haiwezi kukopa bila kupata ushauri kutoka kwake, hivyo madeni yote yanakuwa kwenye usalama na hayawezi kuigharimu nchi.
Vilevile, Profesa Luoga alisema kuwa ni muhimu nchi kukopa kufanya miradi ya maendeleo kwani kwa kutumia fedha za ndani itachukua muda mrefu kukamilisha mradi mmoja, wakati kwa kukopa unaweza kukamilisha ndani ya muda mfupi zaidi.
Ufafanuzi huu unatolewa kufuatia gumzo linaloendelea mitandaoni, ambalo linatokana na ukinzani wa kauli ya Spika Ndugai na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuhusu kuendelea kukopa au kutumia fedha za ndani.
Akiwa katika mkutano mkuu wa pili wa wanakikundi cha Mikalile Ye Wanyusi uliofanyika jijini Dodoma, Spika wa Bunge Job Ndugai alishauri nchi kutumia fedha za ndani kukamilisha miradi ya maendeleo badala ya kutegemea mikopo.
Hata hivyo, jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisisitiza kuwa Serikali yake itaendelea kukopa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya kimkakati na kwamba haitatumia fedha za kodi au tozo za miamala ya simu kukamilisha miradi hiyo.
Rais Samia alisisitiza kuwa deni la Taifa ni himilivu na kwamba mikopo inayotolewa kwa Tanzania ni ile ya masharti nafuu na inalipwa kwa muda mrefu.