Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wamedhamiria kufanya vyema kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho kwa kumaliza kinara wa Kundi D.
Simba SC imepangwa sambamba na US Gendarmerie ya Niger, RS Berkane ya Morocco na Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi amesema wamepanga kuhakikisha kikosi chao kinapata ushindi katika michezo miwili ya mwanzo, kwani ndiyo itawaweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Siku zote michezo miwili ya kwanza ya makundi ndiyo inaamua kama unaenda Robo Fainali au hauendi. Hata msimu uliopita, michezo miwili ya mwanzo ndiyo ilichangia kutufanya tuongoze kundi.”
“Kwa maana hiyo tukishinda nyumbani dhidi ya Asec na kisha ugenini dhidi ya Gendarmerie tutakuwa katika nafasi nzuri ukizingatia michezo miwili itakayofuata itakuwa dhidi ya RS Berkane nyumbani na ugenini,” amesema Nghambi.
Ni mara ya kwanza kwa Simba SC kukutana na RS Berkane na Gendarmerie, lakini imewahi kukutana na Asec Mimosas katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika 2003 ambapo Simba ilishinda bao 1-0 nyumbani na ugenini ikapoteza 4-3.