Moto mkubwa umeoneka ukiwa umeambatana na moshi mkubwa juu ya paa la Bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town asubuhi ya leo, Jumapili.
Kwa mujibu wa mashuhuda, vikosi vya zimamoto vimeonekana katika maeneo ya Bunge hilo kuanzia saa 11.30 alfajiri.
“Paa limeshika moto mkubwa na moshi mzito na Bunge letu linaungua pia,” amesema msemaji wa vikosi vya usalama wa jiji.
“Mpaka sasa moto bado haujadhibitiwa na tunaona ukuta wa jengo linaloungua umeanza kuweka nyufa ukitaka kuanguka,” ameongeza.
Mpaka sasa picha zinaendelea kutumwa kwenye mitandao ya kijamii lakini hakuna taarifa rasmi ya kinachoweza kuwa sababu ya moto huo.
Bunge la Afrika Kusini limehusisha sehemu tatu ikiwemo jengo la mwanzo lililojengwa mwaka 1884, liliongezwa mwaka 1920, na lililojengwa mwaka 1980.
Chanzo cha Moto
Rais Cyril Ramaphosa ametembelea eneo la Bunge la Afrika Kusini linaloendelea kuungua na amesema ni tukio la kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Rais Ramaphosa amesema tukio hilo baya na kushtusha limekuja ambapo nchi inapitia kipindi cha maombolezo ya Askofu Tutu na hata yeye angekuwepo angeshtuka.
Mtu mmoja muhusika wa ulinzi wa eneo la Bunge amehojiwa na vyombo vya usalama na kusema mfumo wa uzimaji moto wa eneo hilo haukua ukifanya kazi vizuri.
Maafisa wa zimamoto wanasema paa la jengo lilikoanzia moto limeanguka lote na eneo kubwa la bunge na viunga vyake vimeungua na mpaka sasa gharama halisi na hasara haijafahamika.