Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Yustino Ndugai amemuaomba radhi Rais Samia pamoja na watanzania wote kwa kutoa kauli ambayo ilizua sintofahamu kuhusiana na hatua za Serikali kuendelea kukopa.
Spika Ndugai ameomba radhi mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Bunge jijini Dodoma.
“Wengi wameumizwa na kauli yangu, wapo waliopata shida ya kutukanwa na wapo waliosumbuliwa waniondoe kwa sababu ya hao wote mimi nimebeba jukumu la kuomba radhi. Nimekosa mimi, nimekosa sana, Mungu anisamehe, watanzania nisameheni, nawaomba radhi,” alisema Spika Ndugai.
Katika kuelezea kauli yake na kuweka sawa juu ya alichokua anataka kuwaelewesha watu, Spika Ndugai amesema nia yake ilikua kuwasisitiza watu waendelee kulipa kodi na tozo za serikali.
“Tarehe 26 kulikua na mkutano wa kinamama wa Mikelile na katika mazungumzo yetu tulikua tunajadili mambo ya maendeleo ya nchi na namna nchi inavyoweza kujikwamua kiuchumi, na nilisisitiza watu walipe kodi, tozo na malipo yote ya serikali ili kupandisha uchumi wa nchi, nia yangu ilikua hiyo tu hakukua na nia yoyote ya kuikashifu serikali,” aliongeza Spika Ndugai.
Spika Ndugai aliendelea kufafanua kuwa baada ya kauli yake ya kuhimiza tozo na kujikwamua kiuchumi yaliibuka maneno mengi ya mitandaoni ambayo yalimuonesha alimkashifu Rais Samia Suluhu Hassan na alishindwa kujibu kwa kuwa alikua anaumwa.
“Sasa wakati yote hayo yanatokea mimi nilikua mgonjwa kitandani, sikuweza kupata nafasi ya kujibu chochote lakini binafsi nimeumizwa sana kuonekana namkashifu Mkuu wa nchi,” alisema.
Katika kuuelezea mkopo wa Sh Trilion 1.3 ambao umefanya miradi ya maendeleo nchi nzima, Spika Ndugai amesema jimboni kwake wamepata fedha nyingi ambazo zimekamilisha miradi mingi ya elimu na kupitia mafanikio hayo anaishukuru serikali ya Rais Samia kwa kuendelea kujali wananchi.
“Haijawahi kutokea fedha nyingi zikaelekezwa kwa wananchi kama awamu hii, sisi Kongwa ukiacha hizo za madarasa bado tuliongezewa milioni 470 kwa shule nyingine mbili za vijijini. Nitakua mtu wa kubeba dhambi kama kwa mafanikio hayo sitamuunga mkono Rais wetu na wabunge wanakuja mtawasikia wenyewe wakisema mafanikio hayo,” Aliongeza Spika Ndugai.
Aidha, Spika Ndugai amesema kuwa haijawahi kutokea utekelezaji wa bajeti ya nchi ukaenda kwa mpangilio kama ilivyopangwa kama mwaka huu wa bajeti wa Rais Samia, huku akisisitiza kuwa kila fedha imeenda sehemu iliyopangwa.
Desemba 26, 2021, akiwa Kongwa Spika Job Ndugai wakati akiongelea umuhimu wa tozo kwa wananchi kiuchumi, alinukuliwa akisema nchi hii ikiendekeza mikopo bila kujitafutia vyanzo vya kipato itauzwa, na baadae Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kusaini mkataba wa SGR, alisema ni lazima Nchi iendelee kukopa ili kuendeleza miradi ya maendeleo.