Spika wa Bunge la Kitaifa nchini Kenya, Justin Muturi, leo Jumatano Januari 5, alipandwa na hasira na kutishia kumfukuza Bungeni, mjumbe ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto.
Muturi alisimamia mjadala baada ya Wabunge kuitwa wakati Mswada huo wa marekebisho ya sheria ya vyama vya kisiasa ukisomwa kwa mara ya tatu, baada ya kiongozi wa wengi wa Bunge la Taifa Amos Kimunya kutoa ombi hilo.
Spika huyo aliyesikika akiongea kwa hasira, alitishia kumtupa nje Mbunge maalum, David Ole Sankok kwa kuzua fujo wakati wa kuwasilishwa kwa mswada huo.
Akirejelea mjadala wa mswada huo uliofanyika Disemba 29, 2021, Spika huyo aligundua kwamba Sankok aliibua suala fulani kwa Spika wa muda, akidai kuwa hapakuwa na muda wakutosha wa kujadili mswada huo wenye utata.
Jambo hili, kulingana na Muturi, lilisababisha Wabunge wengi kukosa kuchangia wakati wa kikao hicho.
“Sankok uliibua malalamiko kwa kusema tunakaribia usiku wa manane. Lazima tuwe na nidhamu ndani ya Bunge hili. Naweza kupata taarifa rasmi na iwapo itadhihirisha kwamba uliiibua swali la kimataifa, utatimuliwa kutoka Bungeni siku ya leo. Huwezi kufanya hivi, maana sivyo mambo yanastahili kuendeshwa,” Muturi alifoka huku Wabunge wakimzomea apewe taarifa kamili ili waidhinishe.
Vurugu na kelele zilianza Bungeni wakati baadhi ya Wabunge walipolalamika kwamba, Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale hakupata muda wa kutosha wa kuwasilisha mapendekezo yake kwenye kikao cha awali.
Baada ya vuta nikuvute, utulivu ulirejea Bungeni na Duale aliwasilisha mapendekezo kuhusu marekebisho yanayostahili kufanya kwenye msada huo wa vyama vya kisiasa.