Klabu ya Newcastle United imefikia makubaliano ya kumsajili Beki wa pembeni kutoka England na klabu ya Atletico Madrid ya Hispania Kieran Trippier.
Newcastle United inayoshiriki Ligi Kuu ya England imekubali kutoa ada ya Pauni Milioni 12 ya kumsajili Trippier, ambaye alijiunga na Atletico Madrid mwaka 2019 kutoka Tottenham kwa Pauni milioni 20.
Jana Jumatano (Januari 05), Trippier alitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya yake, huku akitegemewa kupeleka mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Meneja Eddie Howe.
Trippier amecheza michezo 83 akiwa na Atletico Madrid, ambayo ilishinda Ubingwa wa La Liga msimu uliopita.
Mlinzi huyo alikuwa sehemu ya kikosi cha England ambacho kilifika hatua ya Fainali ya Euro 2020 kipindi cha majira ya joto kilichopita.
Newcastle wanashika nafasi ya pili kutoka chini kwenye Ligi Kuu England, ikiwa imeshinda mchezo mmoja kwenye mashindano yote.