Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC unaangalia uwezekano wa kumsajili nyota wake wa zamani Sharaf Eldin Shiboub, baada yakuonesha uwezo mkubwa kwenye mchezo wa Kombe la Mapinduzi jana Jumatano (Januari 05).
Simba SC ilicheza mchezo wake wa kwanza kwenye michuano hiyo mjini Unguja-Zanzibar Uwanja wa Aman, dhidi ya Selem View ya Pemba iliyokubali kichapo cha mabao 2-0.
Shiboub aliomba kushiriki michuano hiyo akiwa na Simba SC kwa kusudio la kujiweka ‘FIT’ lakini kiwango chake kimeonekana kumvutia Kocha Pablo Franco Martin.
Klabu ya Simba chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ inafikiria kuachana na beki wake kutoka Ivory Coast, Pascal Wawa ili nafasi yake ichukuliwe na kiungo huyo kutoka nchini Sudan.
Wawa alijiunga na Simba Julai Mosi, 2018 akitokea Al Merreikh ya Sudan iliyomsajili kutoka Azam FC msimu wa 2015/2016 mara baada ya mkataba wake kumalizika.
Shiboub aliwahi kuichezea Simba msimu wa 2019/20, kisha akatimkia CS Constantine ya Algeria.
Wakati huo huo klabu ya Simba imethibitisha kuachana na aliyekuwa nyota wake Duncan Nyoni na Abdulsamad Kasim na Ibrahim Ajibu aliyetimkia Azam FC, huku wakithibitisha pia kumtoa kwa mkopo Mlinda Lango Jeremiah kisubi.