Kocha Msaidizi wa Young Africans Cedric Kaze amesema kurejea kwa wachezaji Fiston Mayele, Yanick Bangala na Saido Ntibanzonkia haimaanishi kama wachezaji hao wana umuhimu mkubwa kwenye kikosi chake kuelekea mchezo wa Nusu Fainali ya Mapunduzi dhidi ya Azam FC.

Young Africans itacheza dhidi ya Wanalambalamba hao leo Jumatatu (Januari 10) saa Kumi na Robo (10:15) jioni, ikiwa ni Nusu Fainali ya kwanza kabla ya Simba SC haijapepetana na Namungo FC kwenye Nusu Fainali ya pili kuanzia saa mbili usiku.

Kocha Kaze amesema wachezaji wa Young Africans wote wana hadhi moja, hivyo hatua ya kurejea kwa wachezaji hao watatu kwenye kambi yao huko Unguja-Zanzibar ni suala la kawaida.

“Wachezaji hawa ni sehemu ya timu ya Young Africans, kurudi kwao haimaanishi kwamba wao ndio wana umuhimu mkubwa sana hasa baada ya kuingia Nusu Fainali, kila mmoja ana nafasi ya kucheza.”

“Wachezaji hawa walipewa mapumziko, na muda wao umekwisha, hivyo imewalazimu kujiunga na wenzao kwa ajili ya kuendelea na majukumu ya kuitumikia Young Africans kwa msimu huu.” amesema Kocha Kaze.

Young Africans ilitinga hatua ya Nusu Fainali baada ya kuongoza msimamo wa Kundi B lililokua na timu ya KMKM na Taifa Jang’ombe, huku Azam FC wakiongoza msimamo wa Kundi A dhidi ya timu za Yoso Boys, Namungo FC na Meli 4 City.

Barbara awatuliza Mashabiki, Wanachama Simba SC
Saido aiweka roho juu Young Africans