Baada ya kuibuka Tetesi za Usajili wa Mkopo kwenye klabu ya TP Mazembe, Kiungo kutoka DR Congo na klabu ya Young Africans Mukoko Tomombe amefunguka na kuanika hadharani kila kitu.
Mukoko alitajwa kuuzwa kwa mkopo TP Mazembe siku moja kabla ya dirisha la usajili kufungwa Tanzania Bara, huku kukiwa na makubaliano ya kubadilishwa na Mshambuliaji aliyejiunga Young Africans Ushindi Chiko.
Taarifa zilieleza kuwa, dili la kiungo huyo kujiunga na TP Mazembe lilikufa dakika za mwisho, kufuatia mpango huo kutokuwekwa wazi na viongozi wa Young Africans kwa wanaomsimamia Mukoko, hivyo mpaka sasa anatambulika kama mchezaji halali wa ‘WANANCHI’.
Mukoko amesema mbali ya kufanyiwa taratibu zote ikiwemo kukatiwa tiketi ya kwenda Lubumbashi alishindwa kusafiri kutokana na kushindwa kufahamu hatma yake kwamba anaenda TP Mazembe kama mchezaji wa mkopo au anauzwa moja kwa moja na kumfanya aende moja kwa moja kumuona Bilionea wa GSM.
“Bosi ameniambia nisiende kokote nitabaki hapa Young Africans mpaka mwisho wa msimu utakapomalizika na baada ya hapo ndio kutakuwa na mazungumzo mengine kati yetu,”
“Nimeambiwa keshokutwa nitapewa tiketi ya ndege kwenda kujiunga na timu kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania.” amesema Mukoko
Mukoko aliyejiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu 2020/21 akitokea AS Vita, amekuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza chini ya Kocha Nabi msimu huu 2021/22, huku akibakisha muda wa miezi mitano kwenye mkataba wake.
Hata hivyo imewahi kuelekezwa kuwa, kiungo huyo hatosaini mkataba mpya na klabu hiyo, na badala yake ataondoka itakapofika mwishoni mwa msimu huu.