Kikosi cha Young Africans kimeanza safari ya kuelekea Arusha kupitia Mkoni Kilimanjaro kikitokea Jijini Tanga, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Polisi Tanzania.
Young Africans inaondoka Jijini Tanga, huku ikilamba alama tatu mbele ya Coastal Union waliokubali kibano cha mabao 2-0 jana Junapili (Januari 16), Uwanja wa Mkwakwani.
Hata hivyo taarifa kutoka Young Africans zinaeleza kuwa, kikosi cha klabu hiyo kitaweka kambi mjini Arusha kwa siku tano, kabla ya kutinga mkoani Kilimanjaro kwa mchezo huo ambao utapigwa mwishoni mwa juma hili.
Taarifa hiyo imeendelea kusisitiza kuwa kuna jambo litafanywa mjini Arusha kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, kutokana na wito uliotolewa kwa Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo.
“Wananchi wa Arusha tuna jambo nanyi kesho na keshokutwa, tukutane Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.” Imeeleza taarifa iliyochapishwa kwenye kursa za mitandao ya kijamii ya Young Africans.
Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikijikusanyia alama 32 baada ya kucheza michezo 12 ya Ligi Kuu, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 24, baada ya kucheza michezo 10.