Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara amewajibu waliokua wanaibeza klabu hiyo kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, jana Jumapili (Januari 16).
Young Africans ilikua mgeni wa Wagosi wa Kaya katika Uwanja wa CCM Mkwakwani na kufanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Washambuliaji Saido Ntibanzonkiza na Fiston Mayele.
Manara amesema ilikua lazima waibuke na ushindi katika mchezo huo kutokana na maandalizi kabambe waliyoyafanya juma moja kabla.
”Yaani sisi tukae hapa wiki halafu tufungwe na Coastal Union kweli haiwezekanihaiwezekani, tumejipanga na tumeshinda. Tunawashukuru mashabiki wetu waliokuwa hapa Tanga waliotoka sehemu mbalimbali lakini tunafurahi.
“Dhamira yetu ilikuwa ni kushinda hivyo haijalishi tulikuwa tunafanyaje,walitamba sana waliongea sana wakatuchukulia mazoea wakadhani hii Yanga unaweza kuizoea hii haiwezekani.
“Tulikuwa tumejipanga kupata pointi tatu haijalishi namna gani muda gani tunaweza kufanya, tunaondoka na pointi tatu tunaangalia mechi yetu ijayo,” amesema Manara
Young Africans ilikua na mwenendo mbaya wa kupata matokeo kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani kila ilipocheza dhidi ya Coastal Union tangu mwaka 2016, hali ambayo iliwaibua wadau wengi wa soka ambao waliamini mambo yangeendelea kuwa mabaya kwa ‘WANANCHI’.
Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikijikusanyia alama 32 baada ya kucheza michezo 12 ya Ligi Kuu, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 24, baada ya kucheza michezo 10.