Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson anakibiliwa na kitisho katika utawala wake baada ya wabunge kadhaa wa chama chake kusema watawasilisha baadaye leo barua za kutaka kuitishwa kwa mchakato wa kura ya kutokuwa na imani naye.
Gazeti la Daily Telegraph la Uingereza (UK) limeripoti habari hizo likinukuu duru kutoka ndani ya chama cha kifadhina cha Waziri Mkuu Johnson cha Conservatives.
Taarifa hiyo inasema wabunge 20 wa chama hichohicho wameahidi kuwasilisha barua zao katika wakati hasira ya umma inaongezeka kufuatia ufichuzi kwamba waziri mkuu Johnson alikiuka sheria za kukabiliana na janga la corona.
Kwa mujibu wa taratibu za chama hicho, barua 54 ndiyo zinahitajia kuanzisha mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu na duru zinasema idadi hiyo huenda itafikiwa hivi karibuni.
Johnson analaumiwa kwa kuhudhuria dhifa iliyoandaliwa kwenye ofisi yake ya Mtaa wa Downing mnamo mwaka 2020 wakati Uingereza ilipokuwa imezuia mikusanyiko yote ya umma kukabiliana na janga la Covid-19.
.