Januari 21, 2022 majira ya saa 9 za alasiri, nilikuwa katika viwanja vya Chuo Cha Ushirika Moshi, maandalizi kadhaa ya Tamasha la Utamaduni la Kilimanjaro yakiendelea, niliamua kutoka katika viwanja hivyo kurudi pahala nilipofikia.
Kwa hakika nilifungasha vifurushi vyangu na kutoka uwanjani kuelekea nje ya Chuo cha Ushirika ambapo ningeweza kupata bajaji ya kunifikisha nilipofikia. Nikiwa natoka, nilikutana na wingu kubwa na mara mvua kubwa ikaanza kunyesha. Mvua hiyo ilisababisha mimi kuiacha njia iliyokuwa na lami na kukimbilia katika majengo ya Chuo cha Ushirika Moshi, angalau kujificha mvua.
Japokuwa nilikuwa katika eneo hilo kwa juma zima katika maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la Kilimanjaro, sikujaliwa kupita katika majengo ya utawala au madarasa ya chuo hiki kwa kuwa sikuwa na kitu cha kukifuata.
Mvua hii kubwa ambayo ilinyesha ilinilazimu kupita katika majengo hayo. Nilipofika katika jengo moja baada ya vibanda vya biashara nilikutana na watu wawili, mmoja alikuwa akiwasimamisha wanafunzi na kuwaambia warudi katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika katika maandalizi ya tamasha hilo.
“Haya haya na wewe rudi uwanjani, huko unakwenda wapi.” Niliambiwa na mimi nikamjibu kuwa mimi siyo mwanachuo.
Ndugu huyu ambaye baadaye nilibaini kuwa alikuwa mwalimu alivalia fulana ya rangi nyekundu ambayo ilikuwa na nembo cha Chuo cha Ushirika Moshi. Nilipoyatupa macho yangu kando yalikutana na macho ya mama mmoja anayefahamika kama Jane Mhalila(Muwanji) mumewe anaitwa Nechi Lymo(Mchaga). Jane Mhalila ni dada yangu ambaye nilisoma naye Shahada ya Sanaa ya Habari, enzi hizo Chuo cha Tumaini Iringa.
Jane Mhalila ndiye Afisa uhusiano wa Chuo cha Ushirika Moshi kwa muda mrefu. Kwa wale ambao hawamfahamu Jane Mhalila, yeye ndiye Mtayarishaji wa Kipindi cha Ujue Ushirika, hiki ni kipindi cha redio cha miaka mingi, pengine ni kipindi pekee cha redio kinachoendelea kutayarishwa hadi sasa.
“Chuo cha Ushirika Moshi, kinawaletea-Wananchiiiii tujifunzeniii Ushirikaaaa, Wananchiii tujifunzeni Ushirika.”
Kwa wale wasikilizaji wa RTD zamani watambuka kiashiria hicho cha kipindi cha Ujue Ushirika.
Hakika hata umri wangu mie ninayeandika matini haya, hauwezi kushindana na umri wa Kipindi cha Ujue Ushirika. Nakumbuka pia TANESCO walikuwa na Kipindi cha Bwana Umeme.
“Kwa mwanga safi, Mapishi bila Moshi-Sikilizaa Bwana Umemee.”
Kumbuka nipo na Jane Mhalila, nilimuakia shikamoo! akaitikia marahaba! Akaniuliza mwanangu Makwega siku hizi upo wapi? Nikamueleza nilipo, akaniambia yeye anastaafu mwezi wa tatu, kwa sasa anafanya kazi za mwisho mwisho, anakaribia kuanza likizo ya kustaafau. Nikampa heko kwa kufikia hatua hiyo, akanijibu asante mwanangu Makwega.
Kwa kuwa walikuwa na kazi ya kuhakikisha wanafunzi wanafika uwanjani nilimuaga na nikamwambia mimi ninajificha mvua, akaniambia usikae madarasani nenda pale kwenye jengo la utawala ukapumzike hadi mvua itakapokwisha, ndipo uweze kuondoka. Kweli nilifanya hivyo na kuelekea jengo la utawala la chuo hichi.
Nilifika hapo, kwa kuwa kulikuwa na mvua, nilisogea eneo la utawala ambapo nilikaribishwa na mabenchi mawilii ya mbao moja lilikuwa limejaa watu lakini lingine likiwa tupu.
Nilistaajabu, kabla sijafika katika jengo hilo nilikutana na pahala wanafunzi wengi waliokuwa wamejificha mvua lakini hawakuweza kusogelea mabechi hayo mawili. Nilibaini tu ni nidhamu ya wanachuo hao ilikuwa kubwa ili kuwapa nafasi wageni kukaa katika mabenchi hayo ya utawala.
Nilipokuwa nalishusha begi langu lenye vifaa vyangu vya kazi mgongoni, nilikaribishwa na Mawe ya Msingi Mawili ambayo yalikuwa yamebandikwa chuma chenye maandishi, nilitamani kuyasoma maandishi hayo, niliyasogelea kwa karibu.
“CHUO CHA USHIRIKA-MOSHI, Jengo la chuo hiki limefunguliwa Na Mheshimiwa TAGE ERLANDER Waziri Mkuu wa Sweden, Tarehe 25th Januari 1968.”
Hayo niliyasoma kutoka Jiwe la Kwanza.
Nilililaza begi langu katika benchi hili ambalo lilikuwa tupu, nikaliweka vizuri lisianguke na kuelekeza macho yangu katika jiwe la pili.
“CHUO CHA USHIRIKA-MOSHI Jiwe Hili la Msingi limewekwa Na Waziri wa Biashara na Vyama vya Ushirika Hon A. M. BABU M.P Tarehe 22rd Julai 1966.”
Nilipomaliza kusoma nilishusha pumzi zangu na kutoa kamera yangu na kuyapiga picha mawe hayo vizuri. Kwa uhakika wa kuzipata picha hizo, nilitoa simu yangu na kuyapiga tena mawe hayo ya Chuo cha Ushirika Moshi na cha kusikitisha picha za kamera yangu hazikuwa nzuri kwani kamera yangu ilipata ukungu wa manyunyu ya mvua lakini picha za simu zilikuwa bora sana.
Nilikaa katika benchi hilo la mbao huku nikimtatafakari marehemu Profesa Abdul-rahaman Babu namna alivyokuwa mwanasiasa mzuri mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar, moyo wake wa ujamaa na pia namna alivyopotea katika siasa za Zanzibar na Tanzania.
Nilikumbuka mwaka 1995 namna NCCR-MAGEUZI walivyopendekeza jina la Profesa Babu kuwa Mgombea Mwenza wa Augustino Mrema. Huku likikataliwa kuwa mgombea mwenza wa Urais wa NCCR-MAGEUZI ambacho kilikuwa chama kikubwa cha upinzani wakati huo. Mwaka 1995 NCCR MAGEUZI walifanya mkutano Jangwani mara baada ya Profesa Babu kurudi kutoka Ughaibuni aliongea katika mkutano wa Jangwani ambapo mdogo wangu anayefahamika kama Modestus alishuhudia mkutano huo kwa macho yake aliniambia kuwa.
“Profesa anaongea vizuri sana na anaonekana anazifahamu siasa za Tanzania kwa kina na NCCR MAGEUZI wamesema Profesa Babu ndiye atakuwa mgombea mwenza wa Mrema.”
Lakini mambo hayakuwa hivyo, kupigwa mkasi kwa jina la Profesa Babu kuwa Mgombea Mwenza wa Mrema kulihusishwa na tuhuma kadhaa mara baada ya kuuwawa kwa Sheikhe Abeid Karume.
Nikiwa katika benchi hilo, nilijisemea moyoni kuwa katika maisha ya Profesa Babu, nimejifunza mambo makubwa matatu; kwanza siasa ina upande ambapo mambo huwa yananyooka vizuri sana. Pili, mambo yanabadilika kabisa sawa na yule mtu anayekwenda kuwinda anayeufahamu msitu alafu anapotea msituni, hapo mambo ya siasa huwa yameenda kombo.
Tatu, mambo mema huwa yanajieleza yenyewe, hata kama ubaya utavuma lakini wema unavuma zaidi ya ubaya. Ndiyo maana leo hii mwanakwetu huyu Profesa Babu namkumbuka.
Nilisema haya kwa kuwa natambua sana taifa letu linavyonufaika mno na uwepo wa Chuo cha Ushirika Moshi miaka nenda miaka rudi, hiyo ni sehemu ya kazi ya Ujamaa za Waziri wetu wa Biashara na Vyama vya Ushirika Profesa Abdulrahaman Babu.
Nilitafuta karatasi na kuandika maneno haya;
“Kuna umuhimu mkubwa wa kila kiongozi kufanyia kazi mambo yenye kulenga ustawi wa binadamu, fikiria Profesa aliyesoma Chuo cha ushirika ngazi za chini hadi akawa profesa sasa anaitumia elimu yake kuwasomesha maafisa ushirika wanaokwenda kutoa elimu hiyo katika kila kona za taifa letu,maafisa hao ushirika ndiyo wanaowaongoza ndugu zetu katika vikoba na taasisi zingine za fedha, huo ni ustawi mkubwa wa maisha ya binadamu.”
Kumbuka tu mwanakwetu, nipo katika benchi la utawala la Chuo cha Ushirika Moshi ninajificha mvua. Mvua iliendelea kunyesha kwa saa nzima na mimi nikiwa katika benchi hilo la mbao.
Mara nilipigiwa simu na dada yangu mmoja anayefahamika kama Anita Mwamafupa kuwa uwanjani kuna mkubwa anakuja, hivyo nisogee hapo, nisiwe mbali na uwanja, kweli niliamka na kurudi zangu uwanjani huku nikijisemea moyoni-wema huwa unajipambanua wenyewe, kweli wema huwa unajipambanua wenyewe.
makwadeladius@gmail.com
0717649257