Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin, amewapongeza wachezaji wake kwa kuonyesha kupambana kwenye Michezo ya Ligi Kuu licha ya mambo kuwaendea kombo.

Simba imeambulia alama moja katika michezo miwili iliyopita, ikifungwa dhidi ya Mbeya City FC 1-0, kisha kuambulia alama moja, kufuatia matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema wachezaji wake wamepambana na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga katika michezo hiyo miwili waliyocheza ugenini, lakini bahati haikuwa kwao kupata ushindi.

Amesema ingawa viwanja havikuwa rafiki kwa wachezaji wake na aina ya soka linalochezwa na timu hiyo, lakini walipambana muda wote kutafuta ushindi.

“Ingawa tumecheza vizuri na wachezaji kupambana muda wote kuhakikisha tunapata ushindi, naamini haikuwa bahati kwetu kuondoka na pointi zote katika viwanja vya ugenini,” amesema Pablo.

“Tumekuwa tukicheza mechi karibu karibu, wachezaji wanaumia hakuna jinsi tunapaswa kucheza na tumerudi Dar es Salaam, kujiandaa kabla ya kwenda Kagera kucheza mchezo mwingine wa Ligi Kuu,” amesema Pablo.

Simba itashuka tena dimbani Jumatano (Januari 26), kuvaana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa kiporo utakayopigwa katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Serikali yaagiza maduka ya dawa nje hospitali yaondolewe
Majaliwa atoa maagizo kwa Halmashauri nchini