Serikali ya Bukina Faso, siku ya Jumapili ilikanusha mapendekezo ya mapinduzi ya kijeshi au kwamba rais alikuwa amekamatwa lakini ripoti za vyombo vya habari vya kigeni vinasema, Rais Kaboré alizuiliwa katika kambi ya kijeshi na wanajeshi walioasi.
Milio ya risasi ilikuwa imesikika usiku kucha karibu na ikulu ya rais na kwenye kambi katika mji mkuu, Ouagadougou na video kutoka mji mkuu inaonekana kuonyesha magari ya kivita – yanayoripotiwa kutumiwa na rais – yakiwa na matundu ya risasi na kutelekezwa mitaani.
Huduma za mtandao wa simu za mkononi zimekatizwa, ingawa mtandao wa laini zisizobadilika na wi-fi ya nyumbani zinafanya kazi.
Wanajeshi pia wamezingira makao makuu ya televisheni ya serikali na hakujakuwa na vipindi vya moja kwa moja siku ya leo Jumatatu huku baadhi ya wanajeshi katika taifa hilo la Afrika Magharibi wametaka kufutwa kazi kwa wakuu wa kijeshi na rasilimali zaidi ili kupambana na wanamgambo wa Kiislamu.
Mwandishi wa BBC Simon Gongo ana kwamba “hisia ya hali ya kawaida” imerejea mitaani. Hakuna upigaji risasi zaidi unaoweza kusikika, na watu na magari yanasonga katikati ya jiji.
Umati umekusanyika mbele ya makazi ya kibinafsi ya rais, anasema, “wakitaka kuelewa kilichotokea wakati wa usiku”.
“Bila maoni rasmi kutoka kwa jeshi au serikali, watu wanasubiri kwa hamu taarifa rasmi kuhusu hali hiyo.”
Siku ya Jumapili, mamia ya watu walijitokeza kuwaunga mkono wanajeshi hao na baadhi yao walichoma moto makao makuu ya chama tawala. Amri ya kutotoka nje wakati wa usiku imewekwa.
Haijulikani mahali rais alipo, lakini shirika la habari la AFP lilinukuu vyanzo vya usalama vikisema kuwa yeye na mawaziri wengine wa serikali wako katika kambi ya Sangoule Lamizana katika mji mkuu.
Hakuna mawasiliano kutoka kwa Rais Kaboré mwenyewe tangu Jumapili usiku, alipotuma kwenye mitandao ya kijamii akipongeza timu ya taifa ya kandanda kwa ushindi wao katika mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika.