Kocha Mkuu wa Simba SC Pablo Franco Martin amesisitiza kuendelea kupambana katika Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, licha ya kuwa na matokeo mabaya kwenye mchezo miwili iliyopita.
Simba SC ilipoteza alama tatu dhidi ya Mbeya City ugenini kwa kufungwa bao 1-0, kisha ikambulia alama moja kufuatia matokeo ya sare ya 0-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema bado ana matumaini makubwa kuwa kikosi chake kitarejea katika njia ya ushindi, kama ilivyokua siku za nyuma.
Amesema kwa hakika Ligi Kuu imekua na ushindani mkubwa na kilichotokea ni jambo la kawaida ambalo limewajenga vizuri kwa kuamini chochote kinaweza kutokea katika mchezo wa soka.
Kuhusu mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Kocha Pablo amesema amewaandaa vizuri kisaikolojia wachezaji wake kukabiliana na mchezo huo, ambao utapigwa kesho Jumatano (Januari 26), kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera.
“Ligi imekuwa ngumu, kila timu imejipanga vizuri na sisi tumefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha tunafanya vizuri katika mchezo ujao dhidi ya Kagare Sugar,”
“Utakuwa mchezo wa ushindani kwa sababu katika michezo miwili hatujapata ushindi, tunaendelea kujiimarisha kuelekea mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar.” amesema Kocha Pablo
Mchezo huo ulipaswa kuchezwa Desemba 12 mwaka 2021, lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi kutokana na wachezaji wengi wa Simba SC kukutwa na maambukizo ya ugonjwa wa mafua, kukohoa, kichwa na homa kali, hivyo kusababishwa mechi isifanyike kwenye Uwanja wa Kaitaba.