Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo ametoa rai kwa watekelezaji na wasimamizi wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (Ecosystem Based Adaptation for Rural Resilience – EBARR in Tanzania) unaotekelezwa Kaskazini A – Unguja kuongeza kasi ya uchimbaji wa visima katika eneo la Matembwe ili wakazi wa maeneo hayo waweze kunufaika na maji safi na salama.
Dkt. Jafo ametoa rai hiyo leo 28 Januari 2022 mara baada ya kufanya ziara ya kikazi katika eneo la Matembwe na kuzungumza na watendaji na wasimamizi wa mradi
huo na kuwaagiza kusimamia kazi zote zilizopangwa kutekelezwa na kuhakikisha zinakamilika kwa wakati bila kuomba muda wa nyongeza.
Amesema agenda ya mazingira ni suala linaloigusa dunia kwa sasa na kuainisha kuwa athari za mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na ni mjadala wa kidunia hivyo Ofisi yake itahakikisha inashirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais (Zanzibar) katika kuibua miradi yenye manufaa kwa pande zote mbili za muungano.
“Ndugu zangu sote ni mashahidi wa athari hizi za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ukame na hapa Zanzibar visima viko hatarini kutoweka kutokana na ongezeko la kina cha bahari” Jafo alisisitiza.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt. Saada Mkuya ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza miradi ya maendeleo pande zote mbili za Muungano na kusisitiza kuwa atahakikisha shughuli zilizopangwa kutekelezwa na mradi huo ikiwa ni pamoja na ununuzi wa boti, uchimbaji wa visima na utengenezaji wa majiko banifu unakamilika kwa muda uliopangwa bila kuomba muda wa ziada.
Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini ni wa kipindi cha miaka mitano na ulianza utekelezaji wake 2018 na unatekelezwa katika wilaya za Kishapu, Mvomero, Mpwapwa, na Simanjiro kwa upande wa Tanzania Bara. Kwa Zanzibar mradi unatekelezwa katika Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja – Kijiji cha Matemwe, Mbuyutende na Matemwe Jugakuu.
Lengo la mradi huu ni kuongeza uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia na kuwezesha njia mbadala za kujiongezea kipato. Mradi huu unaratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Kwa upande wa Zanzibar Mradi unatekelezwa kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira (Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais).
Jumla ya shilingi 1,100,112,000 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za Mradi upande wa Kaskazini A, na kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuendesha mafunzo na kuviwezesha vikundi katika maeneo ya mradi kutengeneza majiko sanifu na banifu kwa lengo la kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa na hivyo kupunguza uharibifu wa misitu.
Pia, kuandaa Mipango ya Usimamizi wa Matumizi ya ardhi ili kuwezesha jamii husika kupanga matumizi ya ardhi kwa ajili ya Makazi, Kilimo, Ufugaji, Hifadhi ya Misitu/mikoko na uoto wa asili, hifadhi ya vyanzo vya maji ili kuepusha migogoro katika matumizi ya ardhi.
Kupitia mradi huu utafanyika ununuzi wa boti sita za uvuvi, Uchimbaji wa Visima Virefu sita (6) katika Shehia tatu za Kijini, Mbuyutende na Jugakuu na mpaka sasa jumla ya majiko sanifu 90 yametengenezwa katika kaya ya Matemwe Kijini, Matemwe Mbuyutende na Matemwe Jugakuu.