Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amepanga kukutana na Watendaji Wakuu wa Jeshi la Polisi Januari 31, 2022 ili kujadili jinsi ya kudhibiti mauaji yanayoendelea nchini, amesema katika kikao hicho pia kitajadili jinsi ya kulifanya Jeshi la Polisi kuwa la kisasa katika kudhibiti matukio mbalimbali kiuhalifu nchini. 

Akizungumza katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea Kamisheni ya Uchunguzi wa Kisayansi (Forensic Bureua), jijini Dar es Salaam, Waziri Masauni amesema lengo kuu la kukutana na viongozi hao ni kupata taarifa ya uchunguzi wa mauaji ambayo waliushaanza na kujua jinsi gani matukio hayo yanaweza kumalizwa katika jamii.

“Siku ya Jumatatu nitakua na kikao na Viongozi wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na IGP pale Wizarani kwa ajili ya kupitia matokeo ya kazi ya uchunguzi ambayo wanaifanya na Serikali tunategemea waifanye ili tuweze kuwajulisha wananchi juu ya hayo matukio yote ili tujue tulipofikia, hatua zake ni zipi, na mafanikio yake ni yapi na mikakati kuweza kuhakikisha mambo kama haya ya mauaji tunaweza tukayapunguza katika siku za usoni,” Amesema Masauni.

Ameongeza kuwa, lengo kuu la ziara yake ni kutaka kuona Kamisheni hiyo ya Uchunguzi jinsi inavyochunguza na kudhibiti mauaji pamoja na kuhakikisha wahalifu wanapatikana kwa haraka na kwa ufanisi zaidi. 

Sambamba na hayo yote Waziri Masauni ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wanaosajilia watu laini za simu, wanaochafua viongozi na wanaosambaza picha chafu mitandaoni.

“Wapo watu wamekuwa wakitumia mitandao vibaya kudhalilisha watu wengine, wengine ni watu wazima wanaweza kuwa hata wazazi wao, wapo wanaotumia mitandao kufanya wizi na uitapeli kwa raia wengine, wapo watu ambao wanajadili mambo ambayo yapo kinyume na maadili, desturi za watanzania, ambapo haya yote yanayoendelea kufanyika lazima yadhibitiwe na Jeshi la Polisi, kwahiyo kuna haya ya kuhakikisha haya yote yanafanyika kwa kasi zaidi,” Alisema Waziri Masauni.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhalifu wa Kimtandao, SSP Joshua Mwangasa, alimshukuru Waziri huyo kwa kutembelea Kamisheni hiyo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote aliyoyatoa.

Hakuna wajawazito kutozwa fedha kliniki
TET yatangaza mitaala mipya