Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa ameagiza Halmashauri zote nchini kutekeleza miradi yote ya maendeleo kwa wakati na kuachana na hali ya kufanya kazi kwa mazoea.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo wakati akikagua ujenzi wa ghorofa moja wa makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Geita vijijini unaotekelezwa na SUMA – JKT kwa thamani ya Sh bilioni 2.69.
Waziri Bashungwa amesema hataki kuona kwenye Halmashauri hali ya utekelezaji wa miradi na shughuli za maendeleo zinadolola mpaka Wabunge au wananchi wapaze sauti ili Viongozi waje watoe maagizo ndipo mambo yaanze kutekelezwa.
“Hapa Geita vijiji Rais wetu Samia Suluhu Hassan ameshatuma Bilioni mbili zipo kwa ajiri ya ujenzi wa Halmashauri lakini tatizo ni usimamizi na kutofanya maamuzi kwa wakati, sasa jambo hili hatutalifumbia macho” amesema Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa amewaelekeza Wakurugezi wote nchini kufuata taratibu za kufanya maamuzi ya fedha za umma na kuacha kufanya maamuzi wakiwa katika maeneo ya utekelezaji wa miradi bila kupitia utaratibu wa vikao vya kisheria kama kamati ya fedha ya mipango inayobainisha vipaumbele kwa ajiri ya kupitishwa na baraza la madiwani.
Waziri Bashungwa amewataka SUMA – JKT wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa Jengo la Halmashauri ya Geita Vijijini kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati bila kuathili weledi na kanuni za kitaalam.
Awali, Mbunge wa Geita vijiji, Joseph Msukuma ameeleza hali ya kudolola kwa utekelezaji wa ujenzi wa jengo la Halmashauri huku akilalamikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Geita Vijijini kuchelewa kufanya malipo na kutofuata taratibu za matumizi ya fedha za mradi huo.