Beki kutoka visiwani Zanzibar Ibrahim Abdallah Hamad ‘Bacca’, huenda akakabidhiwa jukumu la kucheza upande wa kulia kwenye kikosi cha Young Africans, kufuatia adhabu inayomkabili beki wa kulia kutoka DR Congo Djuma Shaban.
Djuma Shaban amefungiwa michezo mitatu, kwa utovu wa nidhamu aliouonyesha kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Polisi Tanzania.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Yanga, Thabity Kandoro, Amesema kuwa: “Kuna uhaba wa mabeki halisia wa kulia kwenye kikosi chetu, Kibwana Shomary ni mgonjwa na Djuma amefungiwa, hivyo mwalimu ameamua kumtumia Bacca kwenye eneo hilo.”
“Bacca atakuwa anapishana na Boxer ambaye kwa sasa ndiye beki pekee wa kulia anayecheza kwa ufanisi eneo hilo, ingawa kuna wakati Dickson Job naye hucheza huko kama kukikosekana mbadala.”
Katika mchezowa Jumamosi wa hatua ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Mbao FC, Boxer alianza kikosi cha kwanza akicheza beki wa kulia, huku Bacca akiwa benchi.
Young Africans itacheza mchezo wa mzunguuko wa 14 wa Ligi Kuu Tanzania Bara Jumamosi (Februari 05) dhidi ya Mbeya City FC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.