Uongozi wa Wawakilishi wa Tanzania Kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika Simba SC umethibitisha kuwa Mashabiki 35,000 wataruhusiwa kushuhudia mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Hatua ya Makundi dhidi ya ASEC Mimosas.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo, Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 13, na ilikua inasubiri jibu kutoka CAF kuhusu idadi ya Mashabiki watakaoruhusiwa kuingia Uwanjani siku hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC Ahmed Ally amesema ‘CAF’ imetuma taarifa ya Mashabiki 35,000 kuruhusiwa kwenye mchezo huo leo Jumanne (Februari Mosi).
“Leo Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limetuma taarifa inayoturuhusu kuingiza mashabiki 35,000 katika mchezo huo, kwa hiyo tuwaambie mashabiki wa Simba SC kwamba ni mshabiki hao ndio wataruhusiwa kwenye mchezo huo.”
“Tulitamani Mashabiki waingie kwa wingi na kuujaza Uwanja katika mchezo huo, lakini CAF wametupa idadi ya Mashabiki 35000 ambao wataruhusiwa kushuhudia mchezo wetu dhidi ya ASEC Mimosas.” Amesema Ahmed Ally.
Katika hatua nyingine Ahmed Ally amesema taarifa ya idadi ya Mashabiki walioruhusiwa kuingia Uwanjani siku hiyo ya Februari 13 imeambatana na masharti ambayo yanapaswa kuzingitiwa ili kuepuka maambukizi ya UVIKO 19.
“Yapo Masharti ambayo yameambatana na taarifa hii, ambapo Mashabiki wataruhusiwa kuja uwanjani wakiwa na BARAKOA, Kutakasa MIKONO yao wakifika pale Uwanjani na watatakiwa kuacha nafasi ya siti moja baina ya Shabiki na Shabiki watakaofika Uwanjani.”
“Pia katika mchezo huu haitoruhusiwa kwa Shabiki yoyote kuja na Bango uwanjani, niwafahamishe tu Tiketi siku ya mchezo hazitauzwa uwanjani.”
Baada ya kumalizana na ASEC Mimosas, Simba SC itasafiri hadi mjini Niger kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa pili wa Kombe la Shirikisho dhidi ya US Gendamarie utakaochezwa Februari 20 kabla ya kuikabili RS Berkane ugenini Februari 27.