Joto la Mpambano wa Mzunguuko wa 14 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mabingwa watetezi Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons linaendelea kupanda huku kila upande ukihitaji alama tatu za mchezo huo.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo kesho Alhamis (Februari 03) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa na ukame wa ushindi tangu ilipofanya hivyo dhidi ya Azam FC Januari Mosi.

Akizungumzia mchezo huo Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Patrick Odhiambo, amesema wamefanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kuikabili Simba SC, na ana matarajio ya kupata matokeo chanya.

Odhiambo amesema mchezo utakuwa wa ushindani mkubwa kwa sababu wametoka kupoteza michezo miwili mfululizo, huku wenyeji wao Simba SC wakipoteza dhidi ya Kagera Sugar.

Amesema wamefanya maandalizi mazuri ikiwamo safu yao ya ushambuliaji kuhakikisha inakuwa makini kutumia vema nafasi watakazozipata.

“Tumekuwa na shida kwa washambuliaji wetu, kupoteza umakini, nafasi katika tunazozitengeneza, tumelifanyia kazi na ninaamini mechi itakuwa nzuri kiufundi na kimbinu kwa sababu wote tumetoka kujeruhiwa,” amesema Odhiambo.

Amesema kuelekea mchezo huo atawakosa wachezaji wake wawili, Benjamin Asukile na Jeremia Juma ambao ni majeruhi.

Simba SC ilipoteza mchezo dhidi ya Mbeya City FC kwa kufungwa 1-0 majuma mawili yaliyopita, kisha ikaambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Mtibwa Sugar na kisha ilipoteza dhidi ya Kagera Sugar kwa 1-0.

Urusi yaishutumu Marekani
KMC, Biashara United zapelekwa Azam Complex