Uongozi wa Klabu ya Simba SC umesema kuwa Shilingi Bilioni 20 zilizowekwa na mwekezaji wake Bilionea Mohamed Dewji “Mo” zinaweza kutumika kuombea mkopo wa kujenga uwanja wake itakaoutumia kucheza michezo yake ya michuano yote, ikiwamo Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa.

“Mwanzo ulikuwa ni mpango wa mashabiki waliokuwa na munkari kutokana na jambo lililotokea, lakini wingi wa michango ulifanya viongozi kukaa na kuliendeleza jambo hilo, ndiyo maana kwa sasa tumeandaa michoro ya uwanja, inaundwa kamati maalum ya kulishughulikia suala hilo kwa sababu jambo hili haliwezi kuendeshwa na viongozi au bodi.

Na siyo kama tunategemea michango tu ya wanachama na mashabiki hapana, wao wanaendelea kuchanga, lakini ukumbuke Simba kwa sasa ni taasisi inayokopesheka, tuna kiasi cha Sh. bilioni 20 benki ambazo tukienda kuchukulia mkopo tunajenga uwanja bila matatizo yoyote, kikubwa pumzi tu,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa kwa sasa kuna baadhi ya watu wanaona kama ni jambo ambalo haliwezekani, lakini kwa jinsi viongozi wa klabu hiyo walivyojipanga, wengi watashangaa.

“Tunakwenda kufanya kitu cha tofauti ambacho hakijawahi kuonekana Afrika hii,” amesema.

Kasi ya Simba kutaka kuwa na uwanja wake, ilianza baada ya Desemba 11, mwaka jana, ilipomalizika mechi ya timu hiyo dhidi ya watani zao wa jadi Yanga, huku Ofisa Mtendaji Mkuu Barbara Gonzalez akiwa amezuiwa kuingia uwanjani.
Ni kitendo kilichowaudhi na kuwakera wanachama na mashabiki wa Simba, walioanza kuhamasishana kwenye mitandao ya kijamii kuchangishana pesa kwa ajili ya kujenga uwanja.

Suala hilo lilibebwa na Mshauri wa Mwekezaji, Crescentius Magori ambaye aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa wakiamua hawawezi kushindwa kuwa na uwanja wao japo wa kuingiza watu 30,000 na ndipo mwekezaji mwenyewe, Mo Dewji alipojitokeza na kukubali maoni na maombi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo, akaahidi kutoa kiasi cha Sh. bilioni 2 kuchangia ujenzi huo.

Diamond sio mpenzi wangu
Urusi yaishutumu Marekani