Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons Shaban Kazumba amesema huenda Mshambuliaji Athanas Mdamu akawa sehemu ya kikosi cha Maafande hao wa Jeshi la Megereza, kitakachoikabili Simba SC kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 14 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo kesho Alhamis (Februari 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, saa moja usiku.

Kocha Kazumba amesema Mdamu ni sehemu ya wachezaji wa Tanzania Prisons, hivyo ana kila sababu ya kucheza kwenye kikosi cha timu yao ambayo msimu huu haijaanza vizuri.

“Athanas Mdamu ni sehemu ya kikosi chetu, hivyo kucheza ama kutokucheza kwake ni maamuzi ya benchi la ufundi, lakini niwatoe hofu mashabiki wa Tanzania Prisons kuwa mshambuliaji huyu ana sifa zote za kuikabili Simba SC kesho.”

“Kila Mchezaji ana haki hiyo ya kucheza inategemea na atakavyoamka, hivyo msipomuona Mdamu na wachezaji wengine mfahamu kuna tatizo la kiafya ama changamoto nyingine imetokea, lakini matarajio yetu ni kuwa na kikosi imara ambacho kitapambania alama tatu dhidi ya Simba SC.”

Tanzania Prisons inakwenda kuikabili Simba SC ikiwa inaburuza mkia wa Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuwa na alama 11, huku wenyeji wao wakiwa nafasi ya pili kwa kufikisha alama 25.

Simba SC yaahidi ushindi dhidi ya TZ Prisons
Fiston Abdulrazack: Soka la Bongo linanidai