Maafande wa Ruvu Shooting wamesema hawana njia sahihi ya kujinasua kutoka nafasi za chini kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara zaidi ya kuifunga Mbeya Kwanza FC kesho Alhamis (Februari 03).
Ruvu Shootng itakua mwenyeji wa mchezo huo, huku ikiwa na kumbukumbu ya kutinga hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kuchapa KMC FC kwa mikwaju ya penati mwishoni mwa juma lililopita.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo Jumatano (Februari 02) Jijini Dar es salaam, Kocha msaidizi wa Ruvu Shooting Mohamed Nakuchema amesema, pamoja na kufahamu mchezo dhidi ya Mbeya kwanza utakua mgumu, lakini dhamira yao ni kusaka ushindi ili kujinasua kwenye nafasi ya 15.
Amesema Benchi la Ufundi chini ya Bosi wake Charles Boniface Makwasa limefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo, na wameifuatilia kwa ukaribu Mbeya Kwanza FC na kubaini udhaifu wao.
“Tunajua kwa sasa tupo kwenye nafasi mbaya sana katika msimamo wa Ligi Kuu, njia ya kujiondoa hapa tulipo ni kushinda mchezo wetu dhidi ya Mbeya Kwanza kesho Alhamis, japo tunafahamu hautakua mchezo rahisi.”
“Tumefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo huu, Benchi la ufundi limefuatilia kwa ukaribu michezo ya Mbeya Kwanza FC na limebaini baadhi ya udhaifu, ambao tumeufanyia kazi na ndio maana ninasema hakuna njia mbadala ya kujiondoa tulipo zaidi ya kushinda kwa kutumia udhaifu wao.” Amesema Mohamed Nakuchema.
Ruvu Shooting ipo nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 11 baada ya kushika dimbani mara 13, huku Mbeya Kwanza FC iliyoanza kwa makeke makubwa msimu wa Ligi hiyo, inashika nafasi ya 12 kwa kumiliki alama 12.