Rais wa FC Barcelona, Joan Laporta ameshangaa maamuzi ya Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Ousmane Dembele kuamua kubaki kwenye klabu hiyo hadi mwisho wa msimu huu.

FC Barcelona ilikua tayari kumuuza Dembele mwezi Januari 2022, ili ipate faida ya fedha na kuondokana na mtego wa kumwachia huru yatakapofika majira ya joto (Mwishoni mwa msimu huu).

Klabu za Paris Saint Germain (Ufaransa) na Chelsea (England) zilikuwa tayari kumsajili kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili mwishoni mwa Januari, lakini dili hilo likashindikana.

Laporta ameibuka na kumkosoa Dembele kwani haileti maana ya yeye kubaki kwenye klabu hiyo na kusema; “Tulimpa mapendekezo mawili na yalikuwa mazuri, lakini tunashangaa hakuyakubali.

“Moja lilikuwa kutoka kwenye klabu ya Uingereza, lakini hakutaka kwenda alichagua kubaki hapa kwa miezi sita, si vyema yeye kubaki kwenye klabu, kwa sababu kusaini kwake mkataba mpya ingetupa ahueni ya bajeti ya mishahara.

“Timu ya Dembele ni ngumu kuielewa, Xavi anafanyia kazi kwa ajili ya msimu ujao, tulifikiria kuwa Dembele ameshakubaliana na klabu nyingine, hivyo ndivyo wakala wake alivyotuambia,” amesema Laporta.

Dembele alisajiliwa na FC Barcelona mwaka 2017 akitokea Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa ada ya Euro milioni 105, na mpaka sasa ameitumikia Barca katika michezo 87 huku akifunga mabao 18.

Kocha Young Africans aitamani Mbeya City
Mlinda Lango Tanzania Prisons akataa kuingia mtegoni