Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema vita dhidi ya  ukatili ukiwemo Ukeketaji nchini, inatakiwa kuhusisha watu wa kada zote ili kuleta mafanikio yaliyokusudiwa.

Dkt. Gwajima, ameyasema hayo jijini Dodoma, wakati akizungumza na wandishi wa Habari ikiwa ni kuelekea kilele cha Siku ya kupinga Ukeketaji inayoadhimishwa katika ngazi ya mikoa hasa yenye viwango vya Juu vya  Ukeketaji.

Waziri Dkt. Gwajima

“Hali ya ukeketaji imekuwa inapungua mwaka hadi mwaka kutokana na jitihada za Serikali, asasi za kiraia na wadau wengine wanaoshiriki katika kutokomeza ukeketaji na kubadili mitizamo ya jamii kuhusu mwanamke na mtoto wa kike,” alisema Dkt. Gwajima. 

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa hali ya ukeketaji imepungua kutoka asilimia 18 mwaka 1996 kufikia asilimia 15 mwaka 2010 na asilimia 10 mwaka 2015/16, aidha kupungua huku bado jitihada zaidi zinahitajika hususan kwa Mikoa yenye hali ya juu ambayo ni Manyara yenye asilimia 58, Dodoma asilimia 47, Arusha asilimia 41, Mara wenye asilimia 32 pamoja na Singida ambayo ina asilimia 31. 

Waziri Gwajima, ameitaka jamii ikiwepo kundi la wanahabari kupaza sauti zao kwa pamoja katika vita hiyo, kwa kutumia vyombo vya Habari bila kupotosha kwa kushirikiana na jamii na kuibua changamoto zilizopo ili kuja na majibu ya pamoja yatakayoinusuru jamii na madhila ya uekeketaji.

“Wadau wote wakiwepo wanahabari tuweke mikakati ya pamoja ya kuifikia na kuelimisha jamii katika kufikia malengo ya kupunguza kutoka asilimia 8 iliyopo kwa sasa hadi asilimia 5,” alisema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema, Serikali katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini kwa kushirikiana na wadau wamefanikiwa kuanzishwa kwa Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto 18,618 kwenye Mikoa.

Kaulimbiu ya Siku ya Kupinga Ukeketaji kwa mwaka 2022 ni “Tuongeze Uwekezaji, Kutokomeza Ukeketaji” ambayo inahimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwa pamoja na Tanzania kuongeza uwekezaji wa rasilimali za kutosha ili kutekeleza afua za kuzuia na kukabiliana na athari za ukeketaji ikiwa pamoja na kuwabaini na kuwasaidia wahanga wa ukeketaji katika jamii.

Saudi Arabia kuwekeza kwenye kilimo
Wahariri wapigwa msasa habari za wenye ulemavu