Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa Kimbunga Batsirai katika maeneo ya kusini Magharibi mwa bahari ya Hindi.

TMA imesema Kimbunga hicho tangu kilipojitokeza katika bahari ya Hindi Januari 27, 2022 na kwa sasa kimesogea katika maeneo ya kisiwa cha Madagascar.

Kwa taarifa iliyotolewa jana Ijumaa Februari 4, 2022 na Mamlaka hiyo imesema uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa unaonyesha kutokuwepo kwa uwezekano wa Kimbunga hicho cha Batsirai kufika katika Pwani ya Tanzania.

Imeeleza kuwa uwepo wa kimbunga hicho baharini unatarajiwa kuathiri mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusababisha ongezeko la mvua, vipindi vya upepo mkali unaofika na kuzidi kilometa 40 kwa saa na mawimbi makubwa baharini yanayozidi mita 2 hasa kwa maeneo ya ukanda wa pwani.

Taarifa hiyo imetaja maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua kubwa kutokana na uwepo wa kimbunga hicho baharini kati Februari 4 hadi 8 mwaka huu ni pamoja na mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe na Rukwa.

Hata hivyo mvua za Msimu zinaendelea katika maeneo mengine yanayopata mvua hizo.

TMA imewataka wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka  na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 6, 2022
Maadhimisho ya miaka 45 ya CCM