Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameendelea kuonesha msimamo wake juu ya uchaguzi ujao nchini humo baada ya kuwaambia wabunge wa Jubilee kuwa serikali ijayo itakuwa ya ODM na Jubilee.

Kulingana na waliohudhuria kikao cha Rais Uhuru Ikulu, Kenyatta alisema Jubilee na ODM zitagawana mamlaka iwapo Azimio la Umoja litafanikiwa kuchukua serikali kuanzia Agosti.

Duru zinasema kuwa Rais alisisitiza ni lazima Naibu wa Raila atoke eneo la Mt Kenya na ataanza kumpigia debe Raila baada ya kongamano la Jubilee ambalo litafanyika Februari 25 na 26 katika ukumbi wa KICC.

“Kwa hivyo yule tutakubali kama Jubilee atakuwa naibu wa Raila kwa sababu makubaliano ni mgombea wa urais atoke ODM, na Jubilee itoe mgombea mwenza,” Mbunge wa Kieni Kanini Kega aliambia gazeti la Nation.

Naibu rais William Ruto hata hivyo ameshambulia semi za Rais alipokutana na wajumbe wa Jubilee akisema ni ishara tosha kuwa Uhuru anataka kuwaletea Wakenya project.

Ruto aliyeandamana na kiongozi wa Amani National Congress Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula aliwataka Wakenya kutokubali ‘kupangwa’.

“Tunajua njama ya Rais ya kuchagua mtu anayetaka na kuendelea kutawala serikali jambo ambalo hatutakubali. Wanachagua mtu atakayelinda maslahi na matakwa yao pekee,” alisema Ruto.

Rais Uhuru amekuwa akionekana kumpigia debe Raila kama mrithi wake na hivi majuzi aliwaambia viongozi kutoka Magahribi kuwa yeye si mjinga kuacha naibu wake na kumuunga mkono Raila. Alisema alifikiria sana kabla ya kufanya uamuzi huo ambao umewachoma roho sana wandani wa DP Ruto.

Wakati hayo yakiendelea kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga atakuwa mapumziko ya siku kumi.

Raila alifanya kongamano lake la mwisho la mashauriano mnamo Alhamisi, Februari 3, alipokutana na viongozi kutoka Ukambani wakiongozwa na magavana Charity Ngilu wa Kitui na Kivutha Kibwana wa Makueni.

Duru zilisema kwamba kiongozi huyo wa ODM ataanza ratiba yake kwa kusafiri nchi jirani ya Ethiopia kabla ya kuondoka kuelekea Mumbai, India ambapo ni muwakilishi Mkuu wa Umoja wa Afrika (AU) kwa Maendeleo ya Miundombinu.

Hata akiwa hayupo, kampeni zake za urais za Azimio la Umoja zitaendelea chini ya usimamizi wa Gavana Nderitu Muriithi wa Laikipia, Wycliffe Oparanya wa Kakamega ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM na wanasiasa wengine wakuu wanaoshirikiana na handisheki.

Raila alianza safari yake siku ambayo Rais Uhuru Kenyatta aliwaita wabunge wa Jubilee kwa mkutano wa Jubilee Party Parliamentary Group (PG) katika Ikulu ya Nairobi.

Watoto wafariki kwa kukosa hewa
Wananchi walala juu ya miti licha ya kuwa na anyumba