Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Mara (RC), Ally Hapi pamoja na wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kijitathmini na kuona kama wanafaa kuendelea na nyadhifa hizo au waondolewe.

Ametoa kauli hiyo Jumapili Februari 6, 2022 kwenye hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa maji wa Mugango- Kiabakari wilayani Musoma huku akiahaidi kuzungumzia suala hilo katika mradi wa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.

Rais Samia amesema Mkoa wa Mara una tatizo la kukwama kwa miradi jambo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi akitolea mfano wa miradi iliyokwama kwa muda mrefu kuwa ni pamoja na hospitali hiyo ya rufaa iloyoanza kujengwa mwaka 1974 pamoja na mradi wa umwagiliaji wa Bugwema uliopo wilaya ya Musoma.

“Mkoa wa Mara una tatizo la kukwama kwa miradi mfano mzuri ni ile hospitali ya Mwalimu Nyerere iliyoanza kujengwa miaka ya 70 hadi Serikali ya awamu ya tano ilipoanza kutoa fedha kwaajili ya kuikwamua,” amesema.

Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwl Nyerere

Pia, ameagiza watu waliohusika na ujenzi wa mradi wa makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Bunda vijijini kukaa pembeni kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili ikiwemo rushwa hali iliyopelekea kukwama kwa mradi huo licha ya Sh400 milioni kutolewa kwaajili ya mradi huo.

Amemuagiza RC Hapi kuvunja mikataba ya makandarasi wanaojenga miradi ya barababara za Makutano Sanzte yenye urefu wa kilomita 50 kwa gharama ya zaidi ya Sh60 bilioni pamoja na wa barabara ya Musoma Makojo yenye urefu wa kilomita 5 kwa gharama ya Sh8 bilioni.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara alimwomba Rais kufumua halmashuri za mkoa huo, kutokana na hali ya utendaji wao kutoridhishana Rais Samia amesema kuwa suala hilo lazima lifanyiwe kazi kwani serikali haiwezi kuwang’ang’ania watu wanaokwamisha maendeleo.

“Mkuu wa mkoa ni kama uliota maana leo nilikuwa nimepanga nikufyatue hapahapa bahati yako umeeleza matatizo haya ya kukwama kwa maendeleo ina maana unafanya kazi na matatizo haya unayajua na umeonyesha umechukua hatua gani una bahati,” amesema Rais Samia.

“Mradi mwingine nimeambiwa ni huo wa umwagiliaji wa  Bugwema ambao na wenyewe nao umekwama kuanzia mwaka 1970 lakini niwaambie tunakwenda kufanyia kazi,” alisema Rais Samia.

mradi pic

Amesema kuwa suluhisho la tatizo hilo atalitoa kwa manufaa ya wananchi na kwamba hali hiyo haikubaliki huku akisema kuwa inasikitisha kuona miradi ikikwama wakati wapo viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi wilaya.

“Alipatikana mkandarasi akawa na figisufigisu nikaagiza aondolewe nashukuru Wizara ya Maji mlifanya hivyo na kazi inaendelea niwahakikishie kuwa mradi utakamilika kama ilivyopangwa “amesema Rais Samia

Awali akizungumzia mradi huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema kuwa mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha ziada ya mahitaji ya maji katika vijivi 39 vinayoenda kunufauka ambapo mahitaji ni lita milioni 12 lakini mradi huo utakuwa na uwezo wa kuzalisha lita milioni 35.

Aweso amesema kuwa Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo cha lengo la Serikali la kuhakiksiha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama.

Rais Samia ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Mugango-Kiabakari mradi unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh70.5 bilioni hadi kukamilika.

Mapinduzi ya kijeshi yawashtua viongozi wa Afrika
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 7, 2022