Mwenyekiti wa Bodi ya Utali Tanzania ‘TTB’ Jaji Mstaafu Thomas Mihayo ameipongeza Klabu ya Simba SC, kwa kuendelea kuwa sehemu ya Taasisi iliyojitolea kutangaza Utalii kupitia Michuano ya Kimataifa.
Simba SC imekua Balozi wa Utalii wa ndani na nje ya Tanzania kupitia Michuano ya Afrika, baada ya kuvaa Jezi zilizokua zimebeba ujumbe wa ‘ VISIT Tanzania’ kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu uliopita.
Akizungumza katika hafla maalum ya kutambulisha Jezi zitakazotumiwa na Simba SC kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2021/22, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo amesema hana budi kuwapongeza Viongozi, Wachezaji, Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo kwa kukubali kuwa mabalozi wa Utalii wa Tanzania.
Amesema jambo lolote ambalo lina maslahi na Utalii wa Tanzania ‘TTB’ ipo tayari kutoa ushirikino kama inavyoendelea kufanya na Klabu ya Simba SC ambayo mwishoni mwa juma hili itaanza kucheza michezo ya hatua ya Makundi dhidi ya ASEC Mimosas.
“Jambo lolote ambalo lina maslahi kwetu kama Bodi ya Utalii lazima tulipe ushirikiano, lazima tulishangilie.”
“Simba inapovaa jezi zimeandikwa Visit Tanzania imekuwa na faida sana. Kuvaa jezi hizo kumehamasisha Watanzania na kumekuwepo na ongezeko la watalii kutoka nje ya nchi.” Amesema Jaji Mstaafu Thomas Mihayo.
Simba SC itakuwa mwenyeji wa mchezo huo wa ‘Kundi D’ siku ya Jumapili (Februari 13), utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa kumi jioni.
Simba SC imepangwa Kundi D na klabu za ASEC Mimosas (Ivory Coast), RS Berkane (Morocco) na US Gendermarie (Niger).