Wizara ya Afya imeahidi kutoa ushirikiano na wizara ya Ulinzi katika kuhakikisha mradi wa hospitali ya jeshi inayojengwa kwenye kambi ya jeshi iliyopo msalato inakamilika pamoja na usajili kupatikana kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu katika uzinduzi wa mradi wa hospitali hiyo uliofanyika jijini Dodoma.

“Pia tutaingiza kwenye bajeti yetu ya Dawa mwaka wa fedha 2022/2023 katika mgao wa fedha za Dawa ili hospitali hii ipate Dawa mapema kutoka katika bajeti ya Serikali.” amesema waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amemuomba Waziri wa Ulinzi Dkt. Stergomana Tax kuwezesha mpango wa kufanya upanuzi katika hospitali hiyo uwepo hususan kuweka huduma za kibingwa.

“Tuna hospitali mbili tu Dodoma zinazotoa huduma za kibingwa ikiwemo Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.” amesema Waziri Ummy.

Hata hivyo Ummy Mwalimu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inakusudia kujenga hospitali kubwa ya kibingwa yenye zaidi ya vitanda 500 kwa kuwa uhitaji wa hospitali za kibingwa ni mkubwa mkoani Dodoma.

Kwa upande wake waziri wa ulinzi Dkt. Stergomana Tax amesema kazi ya ujenzi imeshaanza na ujenzi huo unatarajiwa kumalizika mwaka 2024 na itakuwa na vitanda 124.

Naye, Regina Hess ambae ni balozi wa Ujerumani nchini Tanzania amesema ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania umeanza miaka 30 iliyopita na kusaidia katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Dodoma na Dar es Salaam.

Hospitali hiyo itatoa huduma kwa watu wote na itasaidia kuongeza idadi ya wananchi (wagonjwa) kupata huduma katika Mkoa wa Dodoma kutoka wagonjwa 1,683 hadi kufikia 1,807.

Sera ya habari kupitiwa upya
Liunda: Kamati ya waamuzi imewasikia