Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, wamewataka watendaji wa halmashauri hiyo kupitia idara ya elimu kuweka uwiano wa walimu wa kike na kiume katika shule zote za msingi na sekondari.
Hatua ya kudai uwepo wa walimu wa kike katika shule zote, imefikiwa baada ya madiwani wa Viti Maalumu kutembelea shule zote na kubaini kuwepo kwa shule nyingi ambazo hazina walimu wa kike, huku baadhi kukiwa na mwalimu mmoja tu wa kike huku zikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi.
Wakizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha kujadili mapato na matumizi ya fedha katika robo ya pili inayoanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2021, madiwani hao wamesema kuwa hali hiyo inawatesa watoto wa kike maana wanakabiliwa na mambo mengi kutokana na maumbile yao, ambayo ni vigumu kumweleza mwalimu wa kiume.
Mmoja wa madiwani hao Zainabu Shakiru, amesema kuwa suala hilo linasababisha watoto wa kike kuathirika kisaiklojia kwa sababu muda wote wanakuwa wamezungukwa na walimu wa kiume, na kukosa mtu wa kumweleza kwa undani matatizo yao kwa uhuru.