Baada ya kufungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Shilingi laki tano (500,000), Beki wa kati wa Young Africans Dickson Job ameonesha kujutia kosa alilofanya na kupelekea adhabu hiyo kumuangukia.
Job alimkanyaga nyota wa Mbeya City, Richardson Ng’ondya wakati timu zao zilipokutana kwenye mchezo wa mzunguuko wa 14 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Beki huyo aliyesajiliwa Young Africans akitokea Mtibwa Sugar msimu uliopita, amesema ameumizwa na adhabu iliyomuangukia, na hakudhani kama mambo yangekua makubwa kiasi hicho.
Amesema hakukusudia kufanya kosa la kumkanyaga Ngodya, kwani tukio hili lilitokea kama ajali na ndio maana ameshtushwa na maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yake.
“Inaniuma sana, sikudhamiria kufanya vile. Ilitokea tu kama ajali katika mchezo na nimemuomba radhi Ng’ondya na jamii ya wanamichezo wote kwa ujumla, sitarudia kosa kama lile,” amesema Job na kuongeza;
“Kupitia tukio lile nimejifunza, nitaendelea kufanya mazoezi na nikirejea uwanjani naamini nitakuwa bora na kucheza kwa kuzingatia afya ya wachezaji wenzangu.”
Adhabu ya Job iliyotangazwa na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ baada ya Kamati ya 72 kukaa mwishoni mwa juma lililopita, inamfanya beki huyo kukosa michezo dhidi ya Biashara United Mara, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar.