Vita ya ufungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22 inaendelea kuwa ya moto, kufuatia kinara wa sasa Reliants Lusajo kumtumia salamu Mshambuliaji wa Young Africans Fiston Kalala Mayele, akisema amejipanga kuendelea kutupia mabao kwa kila nafasi atakayoipata.
Lusajo ambaye ni nahodha wa Namungo FC, mpaka sasa amefanikiwa kuifungia timu hiyo mabao tisa akifuatiwa na Mayele wa Young Africans mwenye mabao sita.
Lusajo amesema nipo tayari kupambana katika vita ya ufungaji bora msimu huu, ninafurahi kuwa katika kiwango cha kuifungia timu yangu mabao mengi hadi sasa, nitahakikisha ninapambana hadi nichukuwe tuzo ya ufungaji bora msimu huu.
“Nafurahia kiwango ambacho nimekuwa nacho kwa sasa, kama mchezaji hususani ambaye ninahudumu kwenye unahodha ni jambo muhimu kuhakikisha ninaipambania timu yangu ili iweze kupata matokeo mazuri.”
“Kuhusu vita ya ufungaji bora ni kweli hiyo ni sehemu ya malengo ambayo nimejiwekea msimu huu, najua ushindani ni mkubwa kutokana na ubora wa washambuliaji wengine kama vile Fiston Mayele, lakini nimejipanga kutumia kila nafasi ambayo nitaipata kuhakikisha ninafunga mabao mengi zaidi.” Amesema Lusajo