Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo amewaagiza wadau wa mazingira kuzingatia takwimu za hali ya hewa katika kuandaa tathmini za athari kwa mazingira nchini ili kutekeleza matakwa ya sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Waziri Jafo ametoa maelekezo hayo wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 18/02/2022.

“Kila mradi unaotaka kuwekezwa unatakiwa kufanyiwa tathimini za athari za mazingira (EIA), na mchakato wa EIA ni lazima unahitaji takwimu za hali ya hewa, na ikitokea umekosea takwimu utaleta shida”. Amesema Waziri Jafo.

Amesema kuwa sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaipa Mamlaka ya Hali ya Hewa jukumu la kutoa takwimu za hali ya hewa na kuzitaka wizara,taasisi na wataalam elekezi wa mazingira (consultants) kuzingatia umuhimu wa matumizi ya takwimu za hali ya hewa na endapo takwimu hizo zitakosekana inatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kutoka TMA na kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi amesema kuwa warsha hiyo ni fursa muhimu ya kuboresha huduma katika sekta ya mazingira kwa kuzingatia matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na matakwa ya kisheria pamoja na kuimarisha uelewa kuhusiana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.

Aidha, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bi Lilian Lukambuzi amesema NEMC na TMA wameingia makubaliano yenye lengo la kufanya tafiti za pamoja kuhusu masuala ya ya hali ya hewa na mazingira na kufuatilia miradi ya kimkakati ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu.

Naye, mwakilishi wa TEEA Bi. Rukia Ismail alifafanua kuwa warsha hiyo itawasaidia katika kuimarisha ufanisi wa kuandaa thathmini za athari kwa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa mazingira katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa takwimu za muda mrefu za hali ya hewa.

Warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa imeandaliwa kwa ushirikiano wa TMA, NEMC na TEEA ikiwa na lengo la kujenga uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa na umuhimu wa kuzingatia mipango ya utekelezaji wa mipango hiyo.

Muongozo uendeshaji mabaraza ya usululishi
Habari picha: Rais Samia afanya mazungumzo na Rais wa Kamisheni EU